Strategis kuanza kutoa bima mazao ya kilimo

Kamishina wa bima nchini, Dk Baghayo Saqware akizungmza katika uzinduzi wa bima ya jumla iliyoandaliwa na Strategis (Tanzania) Limited

Muktasari:

  • Walengwa ni wakulima na hasa wa vijijini

Dar es Salaam. Kuongeza tija na uhakika wa uzalishaji, kampuni ya bima ya Strategis imetangaza kuanza kutoa bima ya mazao kwa wakulima.

Mpango huo umetangazwa wakati kampuni hiyo ikizindua mpango mpya wa huduma za bima inazozitoa.

Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Kain Mbaya amesema wamekamilisha mifumo ya utoaji bima ya jumla na ndani ya miezi miwili bima za kilimo zitapatikana.

“Kuna changamoto ya kutokuwapo takwimu jumuishi kuhusu kilimo na mazao lakini katika mpango wetu wa biashara tutashirikiana na wizara za fedha na ya kilimo wakati tunasubiri kuimarishwa kwa takwimu hizo,” amesema Mbaya.

Mbaya amesema walengwa wakuu wa mpango huo ni wakulima na hasa wa vijijini watakaofikiwa kidijitali itakapobidi.

Kamishina wa bima nchini, Dk Baghayo Saqware amesema, “Uchumi wa viwanda unahitaji sekta imara ya bima, hivyo kila ubunifu unaofanywa kukuza upatikanaji wa huduma Tira (Mamlaka ya Udhibiti wa Bima nchini) tutauunga mkono.”

Amesema bima kwa wakulima ni hitaji la muda mrefu na Tira ilianza kuwashawishi wakulima kuanzisha bima yao kwa kuzingatia mahitaji lakini hawakufanikiwa.