Sugu aitaka Basata kuiachia TRA kazi ya tozo

Mbunge wa Mbeya Mjini, (kushoto) Joseph Mbilinyi maarufu Sugu akisalimiana na Mhariri Msaidizi wa gazeti la Mwananchi, Florence Majani. Katikati ni Mkuu wa Habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd(MCL) Frank Sanga.

Muktasari:

Mbunge huyo wa Mbeya Mjini alikuwa akizungumzia kanuni mpya za Basata zinazoweka viwango vya tozo kwa ajili ya usajili, maonyesho na kutumika kwa taswira za wasanii katika matangazo ya biashara.


Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu, amesema kazi ya kutoza kodi ni ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na si Baraza la Sanaa (Basata).

Sugu, mmoja wa wasanii wa mwanzo wa miondoko ya rap nchini, pia amesema Basata iachane na kazi ya kufungia wasanii kwa kuwa jukumu hilo ni la mahakama.

Badala yake ameitaka Basata kubakia katika jukumu la kulea wasanii ambalo ndio lengo la kuanzishwa kwa chombo hicho cha Serikali.

Sugu amesema hayo leo (Julai 18) katika mahojiano na MCL Digital alipotembelea ofisi za makao makuu ya kampuni ya Mwananchi Communications zilizopo Tabata.

Msanii huyo wa nyimbo za kiharakati amesema tozo zilizotangazwa katika kanuni mpya za Basata ni kinyume na kazi za msingi za chombo hicho cha Serikali.

Kifungu cha 15 cha kanuni hizo za mwaka 2018 kinaeleza kuwa usajili wa wasanii na shughuli nyingine utakuwa kati ya Sh15,000 hadi sh50,000.

Pia Jedwali la viwango hivyo linaonyesha kuwa gharama za maonyesho na kutumiwa kwa msanii katika matangazo ya biashara ni kuanzia Sh20,000 hadi Sh5 milioni, ikiwa ni pamoja na malipo ya Sh2 milioni za kuandaa matukio ya kiabiasahra na Sh1.5 milioni kwa matukio yasiyo ya kibiashara.

“Nachokiona Basata inatoka katika majukumu yake. Inataka kuingilia kazi ambazo zilipaswa kufanywa na TRA, huku ikiacha zake za ulezi wa wasanii,” alisema Sugu.

Mbunge huyo amesema kuundwa kwa kanuni hizo kunatokana na watendaji wa Basata kutokuwa wasanii na hivyo kutojua changamoto mbalimbali wanazopitia wanaofanya shughuli za sanaa.

Sugu amesema kabla ya kutangaza kanuni na sheria zozote, ni vyema Basata ikakaa na viongozi wa wasanii kuzijadili badala ya kuzitangaza wakati zikiwa zimeshapitishwa, jambo alilosema linaibua manung’inguniko ambayo yangeweza kuipukika.

“Nina wasiwasi watu  waliopewa jukumu la kuiendesha Basata kama wametoka kwenye sanaa kwa kuwa wamekuwa wakitoka nje ya majukumu yao,” alisema Sugu.

“Na walichokifanya cha kuleta kanuni zao hizo, sikubaliani nacho. Lazima wawashirikishe wasanii wenyewe kwa upana ukizingatia wana vyama vyao,” amesema.

Sugu ni mmoja wa wasanii wanaopingana na kanuni hizo ambazo zimeanza kutumika Julai mosi baada ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali.

Hata hivyo, Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alizungumza na viongozi wa wasanii Julai 14 baada ya kuibuka kwa lawama dhidi ya kanuni hizo.

Katika kikao hicho kilichofanyika Uwanja wa Taifa waziri Mwakyembe aliwapa muda wa kwenda kukaa pamoja na kumrudishia mrejesho wa nini wanataka kiboreshwe katika kanuni hizo kabla ya kuanza kutumika.