Sugu apishana na wimbo wake jela

Muktasari:

  • Taarifa ya Basata inasema imefikia hatua hiyo kwa kuwa una maneno ya uchochezi na kuhatarisha amani na utangamano miongoni mwa jamii.

Dar es Salaam. Ikiwa umepita takribani mwezi mmoja tangu mwanamuziki Joseph Mbilinyi maarufu Sugu atoke jela, wimbo wake mpya #219 umekwenda jela baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kutangaza kuufungia jana.

Taarifa ya Basata inasema imefikia hatua hiyo kwa kuwa una maneno ya uchochezi na kuhatarisha amani na utangamano miongoni mwa jamii.

Mbali na kuufungia Basata pia imetoa onyo kwa msanii huyo kuutangaza na kuusambaza kwa watu wengine.

Akizungumzia hatua hiyo, Sugu amesema hana taarifa rasmi za kufungiwa kwa wimbo huo kwani naye amezipata mitandaoni ila atawasiliana na mawakili wake kupata tafsiri ya hicho walichokisema.

Kabla ya kusema hayo kuhusu kufungiwa kwa wimbo wake kwanza alijibu: “Ujumbe umefika,” kisha akaendelea, “Nitawasiliana na mawakili wangu tukapate tafsiri ya hicho wanachokisema mahakamani ikibidi.”

Pia, amefafanua kuwa hakuwa ameutoa rasmi wimbo huo na kwamba alikuwa anajiandaa kuutoa pamoja na video.

Katika wimbo huo wenye beti tatu, mbunge huyo wa Mbeya Mjini anazungumzia harakati zake za kisiasa zilizosababisha afungwe gerezani akiwa mfungwa namba 219.

“Muziki sikuuchagua, bali ulinichagua, nikafanya kweli na dunia ikanijua, nilichofanya kwa hili gemu mnakijua. Mbeya ndiyo inanitesa (wanaitaka Mbeya), najua Mbeya ndiyo inanitesa. Lakini bado napenda Mbeya inavyonitesa,” inasema sehemu ya kibao hicho.

Sugu anasema: “Siasa sikuichagua, amini usiamini siasa ndiyo ilinichagua na iliponichagua Mbeya wakanichagua, kwa mara nyingine tena dunia ikanitambua na wale wasioamini wakaamini imeshakuwa.”

Sugu alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30, 2017 eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya na aliachiwa Mei 10 kwa msamaha wa Rais.