Sugu arudishwa rumande na mwenzake

Muktasari:

Kesi yake kusikilizwa mfululizo

Mbeya. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imezuia dhamana ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga na kuamuru kuendelea kusota mahabusu.

Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite ametoa uamuzi huo leo Ijumaa huku akitoa sababu kwamba kesi hiyo inatakiwa isikilizwe mfululizo kwa muda mfupi na washtakiwa wakiwa wanafika mahakamani hapo wakitokea mahabusu.

“Mahakama hii inataka kusikiliza kesi hii kwa muda mfupi sana, ndani ya wiki moja kuanzia Jumatatu ijayo iwe imeamuriwa, hivyo washtakiwa wataendelea kuwekwa mahabusu,” amesema Mteite.

Sugu na Masonga wameshtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli ambayo waliyatoa katika mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana wakiwa viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.