VIDEO-Sugu kupeleka bungeni siri zilizojificha gerezani

Muktasari:

  • Katika mwendelezo wa mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika jijini Mbeya, Sugu alisema alikuwa anasikilizia hali ya mama yake mzazi, Desderia kabla ya kwenda Dodoma kuanza kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti huku akiwa na siri nzito ya mambo makuu matano aliyotoka nayo gerezani kuhusu wafungwa na askari Magereza.

Mbeya. Leo, Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ atatua bungeni jijini Dodoma kuungana na wabunge wenzake wanaoendelea na vikao vya Bunge la Bajeti baada ya kurejea uraiani akitokea Gereza Kuu la Ruanda alikokuwa akitumikia kifungo.

Sugu na mwenzake, Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya Februari 26, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli waliyoitoa Desemba 30, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Katika mwendelezo wa mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika jijini Mbeya, Sugu alisema alikuwa anasikilizia hali ya mama yake mzazi, Desderia kabla ya kwenda Dodoma kuanza kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti huku akiwa na siri nzito ya mambo makuu matano aliyotoka nayo gerezani kuhusu wafungwa na askari Magereza.

Haki za wafungwa

Sugu anasema akiwa bungeni, atawasilisha masikitiko yake juu ya maisha duni ya wafungwa gerezani ikiwamo malazi, mavazi, chakula na matibabu.

Anasema wafungwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kukosa huduma nzuri. Anasema hawapati chakula cha kutosha na mwenye nguvu ndiye anayeambulia na kwamba baadhi yao hawana sare stahiki na wanakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma za matibabu hata kwa wale wenye bima.

Kilio cha askari magereza

Sugu anasema askari Magereza wanakabiliwa na changamoto nyingi sambamba na kazi ngumu wanayoifanya.

Anasema katika kipindi alichoishi gerezani, aliona baadhi ya askari hususani wenye vyeo vidogo wakijiingiza kwenye biashara zisizo rasmi ili kujikimu.

“Kuna askari wengine wakitoka kazini (gerezani) wanakwenda kubadili nguo na kuchukua bodaboda (pikipiki) wanakwenda kukaa kijiweni kufanya kazi ya udereva wa bodaboda yaani kubeba abiria. Na hawa ninawafahamu kwa sura na majina yao wanaofanya kazi ya bodaboda baada ya kutoka kazini,” anasema Sugu.

Changamoto za kimahakama

Sugu anasema kwa muda aliokaa gerezani amebaini kuwa kuna watu ambao wapo mahabusu kwa miaka mingi kutokana na kesi zao kukosa ushahidi jambo linalofanya Mahakama zisishindwe kuzisikiliza kwa muda mwafaka.

Sugu anasema pia Mahakama zimekuwa zikichelewa kutoa hati za hukumu ambazo zinamuwezesha mfungwa kukata rufaa jambo linalosababisha msongamano magerezani.

“Nakala za hukumu hazipelekwi kwa wakati wala hati za mwenendo wa kesi ilivyoendeshwa hawapelekewi wafungwa gerezani na mtu hawezi kukata rufaa bila kupewa nakala ya hati ya hukumu. Sasa unakuta mtu amefungwa gerezani na amekaa miaka hajapelekewa nakala ya hukumu na anashindwa kukataa rufaa.”

Polisi

Sugu anasema kumekuwa na malalamiko kwamba baadhi ya polisi hawafanyi kazi yao ya upelelezi na uchunguzi kwa weledi na badala yake wamekuwa wakiwafunga watu kwa ushahidi wa kulazimisha ili wakubali kosa.

“Nilichogundua baadhi ya askari wetu hawafanyi uchunguzi wa jambo ili kupata ukweli wa kesi ila wanatafuta ushahidi ili kukufunga hata kama wanajua ukweli kwamba huna kosa, bali umebambikizwa. Kwa hiyo haya ndiyo mambo ninayokwenda kuyasemea bungeni.”