Sumaye: Upinzani kufa si kigezo CCM kutawala milele

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye

Muktasari:

Amesema chama hicho tawala kinapaswa kutambua kuwa vyama vya upinzani ndio vinachochea maendeleo.

Babati. Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema vyama vya upinzani nchini vikifa si kigezo cha CCM kutawala milele na bila hofu.

 

"CCM isidhani kuvikandamiza vyama vya upinzani ni ufahari, upinzani ukifa CCM watashindwa kutekeleza maendeleo kutokana na ukosefu wa demokrasia. Wanapaswa kutambua kuwa vyama vya upinzani ndio vinachochea maendeleo,” amesema Sumaye.

 




ametoa  kauli hiyo jana  Alhamisi Julai 19, 2018 wakati akimnadi mgombea udiwani kata ya Bagara (Chadema), Mathias Zebedayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Ngarenaro mjini Babati mkoani Manyara.

 

Amesema upinzani unapoona jambo halipo sawa hukemea na kuipa nafasi Serikali kurekebisha jambo husika, “kuwa kwenye upinzani si uadui kama baadhi ya watu wanavyodhani.”

 

Amesema wananchi wanapaswa kutambua umuhimu wa demokrasia ya vyama vingi kwani si uhasama, kusisitiza kuwa vyama vya siasa vikishindana kwa hoja, wanaonufaika ni wananchi.

 

“Vyama vitakuwa vinachuana majukwaani na chama kilichopo madarakani kitahofia kupokonywa madaraka hivyo hakitazubaa kitakuwa kinatimiza ahadi zake kwa kuwatumikia ipasavyo wananchi,” amesema.

 

 

Kwa upande wake mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul amesema wananchi wa Bagara wanapaswa kumchagua mgombea wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kwa maelezo kuwa miaka mitatu ya kata hiyo kuwa chini ya diwani wa Chadema, miradi ya maendeleo imeonekana.

 

“Katika mkoa wa Manyara kuna majimbo saba lakini matano yanaongozwa na CCM. Ila hakuna jimbo linalofanana na Babati Mjini ambayo inaongoza kwa kutekeleza shughuli za maendeleo,” amesema.

 

 

Kwa upande wake Zebedayo amesema hawezi kununuliwa kama chakula kama ilivyotokea kwa madiwani wengine waliohamia CCM.

 

“Sitakubali  kuapishwa mara mbili kwenye udiwani yaani eti, niapishwe mwaka 2015 kisha nijiuzulu mwenyewe nihame chama halafu nije tena niwaombe mnichague, hapana sitafanya hivyo," amesema Zebedayo.