Sura tatu za Bulembo

Muktasari:

  • Katika sura ya kwanza katika mchakato huo, Bulembo ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, Machi 9 alisema hatagombea tena nafasi hiyo mbele ya kikao cha baraza la jumuiya hiyo mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Alhaj Abdallah Bulembo ameonyesha sura tatu katika mchakato wa kuwania tena nafasi hiyo.

Katika sura ya kwanza katika mchakato huo, Bulembo ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, Machi 9 alisema hatagombea tena nafasi hiyo mbele ya kikao cha baraza la jumuiya hiyo mjini Dodoma.

Alitumia fursa hiyo kuwaaga wajumbe akisema hoja si ubunge alioteuliwa bali ni utamaduni aliojiwekea katika maisha yake.

Sura ya pili ilijionyesha Julai 2, baada ya Bulembo kuchukua fomu katika mazingira yaliyodaiwa kuwa na usiri, akieleza kutii shinikizo lililokuwa likitolewa na wazee, viongozi na wanachama wa jumuiya hiyo kumuomba agombea kutetea nafasi yake.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya ofisi hizo, Bulembo aliibuka na sura nyingine akieleza kurejea msimamo wake wa kutogombea na tayari ameshaandika barua aliyoiwasilisha kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.

“Leo (jana) nitawasilisha barua yangu kwa katibu mkuu, sitagombea tena ila kwa kuwa bado ni mwenyekiti hadi siku ya uchaguzi, nitabakia kwenye kazi ya kusimamia na kuchuja wagombea. Awali, nilichukua fomu baada ya kushinikizwa na makatibu wakuu na wazee bwana chukua fomu, nikasema tatizo ni fomu tu basi nikachukua,” alisema Bulembo jana katika mkutano wa waandishi wa habari jijini hapa.

Bulembo alisema licha ya kuchukua fomu hiyo, bado hakuwapigia simu makatibu hao kuomba msaada kwa kuwa msimamo wake ni kuwapisha wengine waongoze.

Amesema atabakia kwenye jopo la kuwachuja wagombea wanaotakiwa kuongoza jumuiya hiyo.

CCM ilitangaza kuanza kutolewa fomu kwa wanaohitaji kuwania uongozi kwa ngazi hiyo Julai. Uchaguzi ndani ya CCM na jumuiya zake ni sehemu ya utekelezaji wa kalenda ya chama hicho kwa mwaka 2017.

Uchaguzi kwa jumuiya hiyo na zingine za Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM) unafanyika kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.

“Hoja hapa si ubunge kwamba nitakuwa na kofia mbili, huu ni utaratibu wangu niliojiwekea katika maisha siwezi kung’ang’ania madaraka. Hapa nina vitabu vya kanuni za chama, cha mwaka 2005, 2010, 2012 na 2017, hakuna kipengele kinachozuia kiongozi wa chama kuwania nafasi nyingine ya uongozi,” alisema.

Bulembo alisema kanuni hizo zinaelekeza kiongozi kuchukua fomu na hatima yake itaamuliwa na vikao vya Kamati Kuu ya chama.

Alisema Kamati Kuu itaona kama inafaa, basi itampitisha, lakini huwezi kupitishwa kama hukuchukua fomu.

Bulembo alisema fomu ikishajadiliwa na vikao huwezi kujitoa hivyo amejitoa mapema kabla ya hatua hiyo.

Amesema hatakuwa miongoni mwa wagombea 49 katika uchaguzi utakaoanza Novemba 20 hadi 23.

Bulembo alisema jumuiya hiyo anaiacha katika hali nzuri akiwa amepunguza deni la Sh4.8 bilioni kwa asilimia 65, kununua pikipiki nchi nzima, kuanzisha mradi wa jengo la ghorofa 14 jijini Dar es Salaam na kumaliza kesi 130.

Kuhusu uchaguzi, Bulembo alisema matawi manne kati ya 23,435 bado hayajamalizia uchaguzi, kata 71 kati ya 4,029 hazijamalizia lakini kwa upande wa Zanzibar uchaguzi umekamilika katika majimbo yote 54.

Katika ngazi ya wilaya uchaguzi utaanza kesho, huku ngazi ya mkoa ukipangwa kuanzia Novemba 7 hadi 9.