Sweden yasitisha kumchunguza Assange

  Waendesha mashtaka wa Sweden wameamua kuachana na uchunguzi wa tuhuma za ubakaji zilizokuwa zikimkabili mwanzilishi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Assange, lakini polisi wa Uingereza imeonya akitoka katika ubalozi wa Ecuador alikojificha atakamatwa.

Assange, 45, alikimbilia kwenye ubalozi huo Juni 2012 na amekuwa akiishi humo kukwepa kukamatwa na kurejeshwa Sweden ambako wanawake wawili walilalamika mwanaume huyo kuwanyanyasa kingono, tuhuma ambazo alikanusha.

Lakini zaidi alikuwa akihofia kwamba angechukuliwa na kupelekwa Marekani kukabiliana na mashtaka kutokana na WikiLeaks kuchapisha mfululizo wa nyaraka za siri za kijeshi na kibalozi.

Assange alituma jana ujumbe kwa Twitter kwamba hatawasamehe wala kusahau walioanzisha uchunguzi dhidi yake. "Kuzuiwa kwa miaka saba 7 bila kushtakiwa wakati watoto wangu wakikua na jina langu likikashfiwa. Sitawasahau."

Hata hivyo, polisi mjini London wametoa taarifa kwamba hata baada ya Sweden kuachana na mashtaka dhidi ya Assange, bado ni mtuhumiwa ambaye atakamatwa ikiwa atatoka katika ubalozi huo.

“Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster imetoa hati ya kumkamata Julian Assange kwa kosa la kushindwa kufika mahakamani Juni 29, 2012,” ilisema taarifa.

“Polisi wa Metropolitan wataitumia hati hiyo kumkamata mara akiondoka kwenye ubalozi.”