TB kuchunguzwa kupitia simu ya mkononi

Muktasari:

Huduma ya uchunguzi binafsi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) inamwezesha kila mwenye simu ya mkononi kuchunguza afya yake kwa kupiga *152*05# kisha kuchagua taarifa inayohusu ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Teknolojia katika matibabu nchini inazidi kukua baada Serikali kuzindua huduma za uchunguzi binafsi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Akizungumza leo Septemba 21, 2018 Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema wizara itawezesha ufanisi na ufuatiliaji wa mfumo huo na kuhakikisha taarifa zinakusanywa na kutumika ipasavyo.

“Tutaangalia idadi ya watu waliosajiliwa, idadi ya ujumbe uliotumwa kwa walengwa, idadi ya wagonjwa wa TB waliogunduliwa na ufuatiliaji wa wagonjwa kwa wakati muafaka. Matumaini yangu taarifa zitakazokusanywa zitakuwa muhimu kwa usimamizi wa mtu binafsi na program,” amesema Dk Ndugulile.

Amesema kupitia ujumbe wa uchunguzi binafsi mtu yeyote anaweza kuingia na kujibu maswali kulingana na dalili za ugonjwa wa TB.

Dk Ndugulile amesema baada ya kukamilisha iwapo mteja ana dalili za TB mfumo huo utamwelekeza kwenda kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu na ataendelea kukumbushwa mpaka atakapokubali kwamba ametembelea kituo cha afya.

“Iwapo mteja atagundulika hana TB atashauriwa kujiunga na ujumbe mfupi wa simu wenye kutoa elimu ya TB na aliyegunduliwa atasajiliwa kwenye mfumo wa mtoa huduma za afya. Mpaka sasa watoa huduma kutoka mikoa sita wameshapatiwa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo,” amesema.

Amesema bado changamoto kubwa ni utambuzi wa wagonjwa wapya wa kifua kikuu, wanaoishi na vimelea au wale wanaougua kifua kikuu kwenda kwenye vituo vya afya.

Meneja wa mawasiliano Airtel Tanzania, Jackson Mmbando amesema walianza kwenye wazazi nipendeni meseji milioni 31 zimeingia na zaidi ya akinamama milioni 5 wametibiwa magonjwa ya uzazi kupitia mfumo huo.

“Utaalamu na teknolojia zaidi sisi kama watoa huduma tunazidi kujiimarisha ili kuhakikisha tunasaidia jamii katika masuala ya afya,” amesema Mmbando.

TB inashika nafasi ya 9 kwa kusababisha vifo duniani kote na ni ugonjwa pekee wa kuambukiza unaoongoza ukifuatiwa na VVU.