Friday, July 21, 2017

TBA yapewa miezi 6 kukamilisha ujenzi nyumba ya Jaji Shinyanga

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi; mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Shinyanga. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha ndani ya miezi sita wanakamilisha ujenzi wa nyumba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.

Profesa Mbarawa ametoa agizo hilo jana mkoani humo wakati alipokagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TBA ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kuwapatia waheshimiwa majaji mahali pazuri pa kuishi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kutenda haki kwa wananchi ipasavyo.

“Hakikisheni mnakamilisha ujenzi wa nyumba hii haraka iwezekanavyo ili mheshimiwa huyu apate mahali pazuri pa kuishi, kufanya hivi kutarahisisha majukumu yake na kufanikisha utendaji wa kazi,” amesema Waziri Profesa Mbarawa.

Taarifa iliyotolewa leo Julai 17 na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Uchukuzi imeeleza kuwa Profesa Mbarawa amesisitiza umuhimu wa TBA kuongeza kasi katika miradi mbalimbali inayoendelea ya ujenzi wa nyumba za viongozi ili kuondoa adha ya kodi za pango kubwa zinazopotea kwa viongozi hao kupanga kwa watu binafsi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga Jaji Richard Kibella amemshukuru Profesa Mbarawa kwa niaba ya taasisi zake za TBA na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa namna ambavyo wameshirikiana na mahakama kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kuwapatia huduma nyingine za uendeshaji.

Ameiomba Serikali kukamilisha haraka ujenzi wa nyumba za viongozi na watumishi wa mahakama kwani gharama kubwa zinatumika katika malipo ya upangaji wa nyumba za viongozi.

“Suala la nyumba ni changamoto, nyumba za kupanga zina gharama kubwa na kwa namna moja au nyingine zinaongeza gharama za uendeshaji mahakama na kupunguza usalama”, amefafanua Jaji Kibella.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama hiyo Ernest Masanja, amemueleza Profesa Mbarawa kuwa kukamilika kwa jengo la Mahakama hiyo kumewezesha majaji na watendaji wengine wa mahakama kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na kwa wakati katika kuwapatia wananchi haki.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa hospitali ya mkoa huo unaosimamiwa na TBA na amewataka TBA kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha ujenzi wake unazingatia viwango na ubora na kukamilika kwa wakati.

-->