TBS, FCC kuondoa bidhaa feki

Muktasari:

  • Lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu kuhusu majukumu ya taasisi hizo.

Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), zimezindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu bidhaa bandia.

Lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu kuhusu majukumu ya taasisi hizo.

Kampeni hiyo ya miezi miwili inatarajiwa kufanyika katika maeneo ya Kanda ya Kati; Kaskazini; Nyanda za Juu Kusini; Ziwa; na Kusini.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari juzi, ofisa mwandamizi mawasiliano na uhusiano wa umma FCC, Frank Mdimu alisema maofisa wa taasisi hizo watawafikia wadau kupitia redio za kijamii, mikutano na wanahabari na jumuiya za wafanyabiashara.

Naye ofisa mwandamizi wa kitengo cha mawasiliano TBS, Rhoida Andusamile alisema kuna uelewa mdogo kuhusu dhamana ya kuwalinda walaji, hivyo kampeni hiyo ni muhimu ili kufikia malengo ambayo ya taasisi. Taasisi hizo zimekuwa zikifanya ukaguzi wa bidhaa kwa pamoja kwa ajili ya kumlinda mlaji.