TCD wataka kumwona Rais, wadai Katiba mpya

Muktasari:

  • Akisoma mapendekezo ya mkutano huo, Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amesema mbali na Katiba mpya kuna haja ya kujenga taasisi imara za usawa na haki.

Kongamano la viongozi wa siasa na viongozi wa dini lilikoandaliwa na Kituo cha Demokrasia (TCD), limemalizika leo jijini Dar es salaam, huku wajumbe wakipanga kwenda kumwona Rais John Magufuli wakiwa na pendekezo la kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba.

Akisoma mapendekezo ya mkutano huo, Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia amesema mbali na Katiba mpya kuna haja ya kujenga taasisi imara za usawa na haki.

"Umoja wa kitaifa utaondoa dosari mbalimbali ambazo hivi karibuni umeleta migogoro. Kuna umuhimu wa kuendeleza mchakato wa Katiba kwa  masilahi ya Taifa," amesema Mbatia.

Ameongeza: "Kituo cha Demokrasia kwa sababu ndio jukwaa la kutolea maoni. Tutafanya mazungumzo na Rais ili ili kuangalia mwelekeo wa jukwaa hili."

Ameitaja mapendekezo mengine kuwa ni kuimarishwa kwa Uhuru wa kutoka maoni na kuwataka wadau wa siasa kujiepusha na siasa za chuki.

Hata hivyo, mjumbe wa CCM katika mkutano huo, Wilson Mukama amesema Katiba mpya siyo kipaumbele cha Serikali ya sasa.

Mukama aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho alitoa mfano wa Kenya alisema licha ya kuwa na katiba mpya imeendelea kuwa na vurugu.