Hatima ya Times FM mahojiano na Diamond, wiki hii

Muktasari:

Machi 22, 2018, Times ilipokea barua ya kuwataka wawasilishe kipindi hicho kilichorushwa Machi 19, 2018 na kutii agizo hilo.


Dar es Salaam. Hatima ya Kituo cha Redio Times cha jijini Dar es Salaam kilichotakiwa kuwasilisha kipindi cha mahojiano waliyoyafanya na mwanamuziki Diamond Platinumz kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ajili ya uchunguzi zaidi, itajulikana wiki hii.

Taarifa zilizoifikia MCL Digital leo Jumatatu Machi 26, 2018 zinaeleza kuwa kamati ya maudhui ya TCRA iliyokuwa ikifanya uchunguzi huo inakaribia kumaliza kazi hiyo.

Machi 22, 2018, Times ilipokea barua ya kuwataka wawasilishe kipindi hicho kilichorushwa Machi 19, 2018 na kutii agizo hilo.

Mwanamuzi Diamond alizua mjadala baada ya kuzungumzia suala la nyimbo za wasanii hao kufungiwa akimlalamikia Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kutowatendea haki wasanii.

Ofisa Mkuu Idara ya Utangazaji wa mamlaka hiyo, Andrew Kisaka ameieleza MCL Digital leo kwamba tayari kamati ya maudhui inakaribia kumaliza kazi yake ya kupitia maudhui ya kipindi hicho.