TFDA kutokagua bidhaa, dawa zenye kibali cha ZFDA

Muktasari:

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imesema haitarudia kukagua bidhaa za chakula na dawa zitakazokuwa na kibali cha ukaguzi cha Zanzibar


Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imesema haitarudia kukagua bidhaa za chakula na dawa zitakazokuwa na kibali cha ukaguzi kutoka Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi  Oktoba 18, 2018 na meneja wa TFDA kanda ya Mashariki,  Emanuel Alphonce katika mkutano na wadau wa uagizaji bidhaa za chakula na dawa.

Amesema wazalishaji bidhaa wa Zanzibar ambao bidhaa zao zimekaguliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) sasa wataziingiza Tanzania Bara bila kufanyiwa ukaguzi na TFDA.

“Bidhaa zote za chakula na dawa zitakazokaguliwa na kupewa cheti an ZFDA hazitakaguliwa tena Tanzania Bara. Nasisitiza zinazozalishwa si zilizoagizwa nje na zikapitishiwa huko kuja huku,” amesema Alphonce.

Mbali na hilo amesema viongozi wa TFDA na ZFDA wameanzisha mpango wa kufanya kazi pamoja ili bidhaa zinazozalishwa pande hizo mbili zikaguliwe upande mmoja ili kuondoa usumbufu.

Mkurugenzi wa huduma za dawa wa Wizara ya Afya ambaye pia ni Famasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema wanashirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha  kunakuwa na mwendelezo wa upatikanaji bidhaa zitakazouzwa kwa bei nafuu.

Amesema Serikali inaendeleza mazungumzo, majadiliano ikiwamo mkutano huo kupata maoni ya wadau juu ya nini kifanyike ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kumfikishia mlaji bidhaa zenye ubora, bei nafuu na kwa wakati.

Katibu mkuu wa Chama cha Mawakala wa Mizigo Tanzania (Taffa), Tony Swai amezungumzia mamlaka za Serikali kuhusika katika urasimu wa utoaji bidhaa bandarini.

Ameutaja urasimu huo kuwa ni pamoja na kucheleweshwa utoaji wa nyaraka na vibali mbalimbali kwa ajili ya kutoa mizigo.

Amesema mfano mtu anaweza kufuatilia kibali kwa muda mrefu huku viwanda vikikosa malighafi na kulazimika kufungwa.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga amesema licha ya kuwapo malalamiko, kampuni nyingi zinazosafirisha na kuagiza bidhaa hazitii sheria zinazosimamia biashara ya kuagiza, ikiwamo kufanya ulaghai.

Amesema kuanzia Novemba, 2018  TBS itazindua dirisha la kupokea maombi mtandaoni ili kuwapa fursa wateja kutuma nyaraka na malalamiko kupitia mfumo wa mtandao.