TFDA yakamata kilo 7,500 za samaki wabovu kutoka nje

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza akizungumza na mmiliki wa Kampuni ya Sais Boutique iliyopo Tabata Bima, Dar es Salaam, Sadick Mapolo wakati maofisa wa TDFA walipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maghala ya kampuni hiyo na kubaini samaki wabovu kilo 7,500 aina ya vibua kutoka nje ya nchi waliokutwa wameharibika.

Muktasari:

  • Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imekamata kilo 7,500 za samaki aina ya vibua walioharibika ambao waliagizwa na Kampuni ya Sais Boutique kutoka China, Julai mwaka huu.

Taarifa ya kuwapo kwa samaki hao sokoni iliripotiwa na Gazeti la Mwananchi Jumapili, Jumapili iliyopita ikieleza kuwa walikuwa wakiuzwa kwa bei ya chini na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kimataifa la Feri, Dar es Salaam.

Akizungumza jana Tabata Bima, Dar es Salaam ambako samaki hao wamehifadhiwa, Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema mamlaka hiyo ilianza kufanya uchunguzi baada ya kuona taarifa kwenye gazeti hili ikiwa ni pamoja na kwenda katika Soko la Feri ili kujua namna wanavyoingizwa nchini.

“Samaki hawa ni wabovu lakini walikuwa wanauzwa mitaani kwa bei ndogo na tulimkuta mmoja wa wasambazaji akiwa na maboksi 10 ya samaki walioharibika baada ya kumbana ndipo alituelekeza anapowanunua ikabidi tuje kwa ajili ya kuhakikisha na ndipo tukawakamata wahusika,” alisema Simwanza.

Alisema bei ya kawaida ya samaki aina ya vibua ni Sh30,000 mpaka Sh35,000 kwa boksi moja la kilo 10 lakini mfanyabiashara huyo alikuwa anawauza kwa Sh23,000.

Alisema walipofika katika eneo hilo walikuta makontena mawili, moja lilikuwa limejaa samaki ambao walionekana kuwa wazima huku lile lililokuwa nusu lilikuwa na samaki walioharibika kutokana na kutoa harufu na kuzingirwa na inzi.

Simwanza alisema Kampuni ya Sais Boutique ilipewa kibali cha kuingiza samaki Julai 8, mwaka huu na kwa mujibu wa taratibu za TFDA, kila mfanyabiashara mwenye kibali anapoingiza bidhaa anapaswa aipeleke ikaguliwe kabla ya kuiingiza sokoni ili kujiridhisha kama inafaa kwa matumizi ya binadamu.

Alisema kampuni hiyo ilikiuka taratibu hizo na kuanza kuuza samaki hao kabla hawajakaguliwa na kusema kwamba kufanya hivyo ni kosa kubwa.

Alisema kutokana na kosa hilo, mmiliki wa kampuni hiyo, Sadick Mapolo yuko chini ya ulinzi akisubiri kuchukuliwa hatua za kisheria kulingana na kosa alilofanya huku taratibu za kuteketeza bidhaa hiyo zikifanyika.

Alisema eneo ambalo linatumika kuhifadhia na kuuza samaki hao siyo rasmi kwani halikusajiliwa na TFDA.

“Hapo alipo ana kosa jingine kwani amehifadhi chakula hiki katika sehemu isiyo salama. Angalia kontena zilizowekwa samaki hawa zimezungukwa na gereji. Tulivyofika tulihisi kumehifadhiwa mizigo tu ya kawaida, hatukudhani kama kuna chakula,” alisema Simwanza.

Maofisa wa TFDA walichukua sampuli ya samaki aina ya Kolekole ambao wametokea Yemen waliopo katika kontena ambalo lilikuwa halijaanza kuuzwa lenye kilo 27,500 ili kuwapima.

Akizungumzia sakata hilo, Mapolo alisema samaki hao waliingia nchini kwa kufuata taratibu zote na kwamba kontena lililokamatwa awali, lilikuwa na kilo 22,500 na kilo 15,000 kati ya hizo zilishauzwa kwa watumiaji. “Samaki hawa waliingizwa Julai, mwaka huu wakiwa katika hali nzuri lakini kutokana na matatizo ya umeme na uhifadhi, samaki 500 kati ya 7,500 waliobaki waliharibika,” alisema Mapolo.

Alisema samaki hao walikuwa wanauzwa kwa wafanyabiashara wa Soko la Feri kwa bei ya jumla ya Sh23,000.

Mapolo alisema baada ya kuona baadhi ya samaki wameanza kuharibika alikuwa katika harakati za kuwaondoa lakini kabla ya kufanya hivyo maofisa wa TFDA wakatokea na kumkamata.