TFDA yateketeza bidhaa feki Tabora

Vipodozi mbalimbali kabla ya kuharibiwa na TFDA mjini Tabora.Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Bidhaa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh32milioni zimeteketezwa mkoani Tabora leo Jumamosi Septemba 22, 2018 na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)

Tabora. Bidhaa mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh32milioni zimeteketezwa mkoani Tabora leo Jumamosi Septemba 22, 2018 na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Meneja wa TFDA kanda ya Magharibi, Dk Edgar Mahundi amesema vipodozi vilivyoharibiwa vilikuwa na viambata vya sumu na kwamba havifai kwa matumizi.

Kwa upande wa vyakula amesema muda wake wa matumizi ulikuwa umekwisha, kubainisha kuwa dawa zilizoteketezwa zilikuwa za mifugo na hazikusajiliwa na mamlaka hiyo.

Dk Mahundi amewataka wafanyabiashara kufuata sheria, kanuni na taratibu katika biashara zao ili kutokuwa na bidhaa zitakazoleta madhara kwa watumiaji.

Ofisa afya na usafi wa mazingira manispaa ya Tabora, Paschal Matagi amewataka wafanyabiashara kuacha ujanja katika biashara zao ili kuepuka hasara kwa bidhaa zao kuharibiwa.

Akizungumzia tukio hilo mfanyabiashara wa dawa za mifugo, Ngemela Kitapondya amesema walinunua dawa hizo bila kufahamu kuwa zimesajiliwa na kuishauri mamlaka hiyo kutoa elimu.