TLS bado yakuna kichwa mabadiliko kanuni za uchaguzi

Muktasari:

Ni kutokana na mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa uongozi wa chama hicho yaliyofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)


Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi amesema bado hawajafanya uamuzi wowote juu ya mabadiliko ya masharti ya kugombea uongozi wa chama hicho.

Ngwilimi ametoa kauli hiyo baada ya Machi 10, 2018,  TLS kudai kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) imeongeza masharti katika mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa chama hicho, yanayowanyima fursa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi wowote wa chama hicho.

Akizungumza na MCL Digital leo  Machi 15, 2018 Ngwilimi amesema: “Bado hatujafanya uamuzi, tunasubiri ushauri wa mawakili wetu kupitia kamati za TLS.”

Ngwilimi amesema mara baada ya kushauriwa kipi cha kufanya watawaeleza Watanzania na wanachama wao huku akiwataka kusubiri.

Uchaguzi wa TLS unatarajiwa kufanyika katika mkutano mkuu wake Aprili 13 na 14, 2018. Kwa sasa rais wa chama hicho ni Tundu Lissu aliyepo Ubelgiji kwa matibabu baada ya Septemba 7, 2017 kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 nje ya makazi yake mjini Dodoma.