TMA yatahadharisha wasafiri wa majini

Muktasari:

Mikoa ya Pwani na Kanda ya kati imekuwa na upepo mkali unaoambatana na kutimka vumbi, jambo ambalo limetolewa tahadhari na TMA ikiwamo kuwataka wananchi  na wanaotumia usafiri wa majini kuchukua tahadhari

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi na wanaotumia usafiri wa majini kufuatia kuwapo kwa upepo mkali.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Oktoba 23, 2018, Samwel Nguya kutoka kituo kikuu cha utabiri cha TMA amesema watu wawe makini na mamlaka zinazoshughulika na usafiri wa majini ziwe makini kwa kuchukua tahadhari kuhakikisha hakuna maafa yanayoweza kutokea.

Amesema upepo huo unatokana na kuimarika kwa hali ya hewa kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika na mfumo wa upepo wa Kusini.

Nguya amesema upepo huo mkali utavuma kwa siku tatu kwenye Ukanda wa Pwani ya Bahari ya  Hindi na maziwa yote makuu ikiwamo Nyasa, Viktoria na Tanganyika na mikoa yote iliyopakana na maeneo hayo, ikiwamo na mikoa ya kanda ya kati.

“Tunaendelea kufuatilia mwenendo wa upepo huo na kutoa tahadhari kila inapolazimika kufanya hivyo, wanaotumia vyombo vya maji wachukue hatua ikiwamo mamlaka zinazohusika na usafiri wa majini,” amesema Nguya.