Saturday, September 23, 2017

TPA yaipa upendeleo Rwanda

 

By Ephrahim Bahemu ebahemu@mwananchi.co.tz

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imesema imetenga eneo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya Rwanda katika bandari kavu za Kwala na Ruvu ikiwa ni kuimarisha uhusiano wa biashara.

Pia, mamlaka hiyo imesema imekamilisha ujenzi wa ofisi nchini Rwanda na inachosubiri ni ufunguzi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alipokutana na Balozi wa Rwanda nchini, Eugene Kayihura alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam juzi.

“Kuwapatia sehemu ya kuhifadhia mizigo na ufunguzi wa ofisi kutasaidia kuimarisha huduma kwa wateja wetu wanaotumia bandari yetu kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Kakoko alisema shehena ya Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka mitano, imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 9.9 kwa mwaka. Imeongezeka kutoka tani 630,000 mwaka 2012/13 hadi tani 950,000 mwaka 2016/17.

Alisema hivi karibuni alikutana na wafanyabiashara wa Rwanda waliomweleza wanaridhishwa na huduma za bandari wanazopatiwa, hivyo hana budi kuziboresha zaidi.

Aliwaomba wafanyabiashara kutumia Bandari Kavu ya Isaka, ili kupunguza umbali wa safari kufuata mizigo Dar es Salaam.

Naye Balozi Kayihura aliishukuru Tanzania kwa kuwapatia eneo la kuhifadhia mizigo na kwamba, biashara kati ya nchi hizo inakua kwa kasi kutokana na kuimarishwa kwa huduma za bandari.

“Asimilia 90 ya mizigo yote inayoingia na kutoka Rwanda inapitia Bandari ya Dar es Salaam. Jambo hilo linaashiria uhusiano mzuri wa biashara,” alisema.

Alisema hata ziara yake hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano wa biashara.

-->