TPB yajipanga kuwasaidia wenye kipato kidogo

Muktasari:

  • Mradi huo unaoitwa ‘Digitalizing Informal Savings Mechanisms’ utakaoendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu, utawawezesha wateja kupitia vikundi vyao kuweka akiba na hata kukopa kupitia simu zao za mkononi.

Benki ya Posta Tanzania (TPB) imeungana na taasisi ya Savings at the Frontier (SatF) katika mradi utakaogharimu Sh2.2 bilioni kwa ajili ya kusaidia wananchi kutoka mikoa ya pembezoni, hasa  wenye vipato vidogo wanaokabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za kifedha.

Mradi huo unaoitwa ‘Digitalizing Informal Savings Mechanisms’ utakaoendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu, utawawezesha wateja kupitia vikundi vyao kuweka akiba na hata kukopa kupitia simu zao za mkononi.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Februari 16, 2018 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi amesema mradi huo utaanzia mkoa wa Ruvuma na baadaye mikoa ya Mtwara, Lindi, Njombe, Iringa na Morogoro.

Amesema kupitia mradi huo, TPB inatarajia kuwaunganisha kwenye mfumo rasmi wa kifedha wateja wapya 300,000 hadi kufikia mwaka 2020.

“Watanzania wengi waishio kwenye mikoa ya pembezoni, hususani wenye vipato vidogo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa huduma za kifedha,” amesema,

“Kupitia ushirikiano huu na SatF, TPB itawawezesha wananchi kupitia makundi au mtu mmoja mmoja, kujiwekea akiba kupitia teknolojia rahisi na salama isiyowalazimu kwenda kwenye tawi la benki ili kupata huduma hizo za kifedha."

Kwa upande wake, Meneja wa mradi wa programu ya SatF nchini Uingereza, Steve Peachey, amesema TPB ndio benki ya kwanza kufanya kazi na taasisi yake hapa nchini, na walivutiwa na namna ambavyo imeonyesha dhamira ya dhati kuwasaidia wananchi hao kupata huduma za kifedha.

“SatF ni programu maalum yenye malengo ya kuhakikisha huduma za kifedha za uhakika zinawafikia wananchi wengi walio nje ya mifumo rasmi ya kibenki,”amesema.

“Programu hii inaratibiwa na shirika la Oxford Policy Management kwa ufadhili wa taasisi ya kimataifa ya MasterCard Foundation, dhumuni kuu ikiwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na jamii zenye vipato vya chini kwenye nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.”