TPSF yaibebea bango gesi asilia kwa viwanda

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imewataka wadau wa mitambo ya uzalishaji umeme, gesi na mafuta kujenga viwanda hivyo nchini.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya mitambo na mashine za uchimbaji wa rasilimali hizo yatakayofanyika nchini na kushirikisha zaidi ya mataifa 25 ikiwamo Misri, Uturuki, India na Japan. “Wasiegemee kuleta bidhaa tu kutoka nje na kuziuza nchini, bali wafikirie namna ya kuanza kujenga viwanda ili baadhi zitengenezwe hapa kwa kutumia gesi asilia,” alisema Simbeye.

Simbeye alisema ugunduzi wa gesi asilia mkoani Mtwara, Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kuyafanya rafiki itakuwa kichocheo cha uwekezaji wa miradi mikubwa yenye manufaa mengi kwa jamii.

Maonyesho hayo ya 20 yalishirikisha kampuni za magari ,ambazo zilishauriwa kufikiria kuzalisha magari yanayotumia gesi ili kuongeza matumizi ya rasilimali hiyo na kupunguza matumizi ya mafuta.

Mpaka sasa zaidi ya futi trilioni 57 za ujazo wa gesi asilia zimegundulika na tayari kampuni na taasisi zaidi 70 zimeunganishwa kwenye matumizi jijini Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Mauzo wa Kampuni ya Hyundai, Betty Kibasa alisema ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kununua bidhaa zao, wamezindua mfumo mpya unaowaruhusu wateja kulipa asilimia 50 na kumiliki gari.

“Mteja atalipia nusu ya bei, inayobaki anaweza kupewa mkopo kutoka benki au kwetu na kukamilisha ndani ya miezi sita hadi miaka mitatu,” alisema Kibasa.