TRA yaeleza sababu ya kutekeleza theluthi moja ya bajeti

Muktasari:

Imeelezwa kuwa asilimia 70 ya Watanzania waliopo vijijini hawalipi kodi

 

Dar es Salaam. Taarifa ya makusanyo ya Serikali iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) juzi, imebainisha sababu nyingine ya kutekelezwa kwa theluthi moja tu ya bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha.

Kwa mwaka mzima ulioishia Juni 2017, TRA imekusanya Sh14.4 trilioni ikiwa ni pungufu kwa Sh700 bilioni za lengo la Sh15.1 trilioni. Pamoja na kutofikiwa kwa lengo, TRA imesema makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 7.6 jambo linaloelezwa kuwa si la kujivunia.

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja amesema makusanyo hayo yanaakisi vyanzo vinavyowategemea watu wachache. Amesema kiasi kilichopanda ni kioo cha uchumi wenye wigo mdogo wa ulipaji kodi kwa kuwa takriban asilimia 70 ya Watanzania waliopo vijijini hawalipi kodi licha kipato wanachotengeza.

Kuhusu kutotekelezwa kwa bajeti kwa kiasi kilichotarajiwa hivyo kuathiri miradi mingi ya maendeleo, taarifa za Wizara ya Fedha na Mipango ilieleza kulitokana na kuchelewa kwa fedha zilizoahidiwa na wahisani na Serikali kutokopa kutoka taasisi za kimataifa.

Mbunge wa Vwawa (Chadema), David Silinde amesema takwimu zilizotolewa na TRA ni za jumla kwa kuwa hazijaainisha vyanzo vilivyochangia mapato hayo.

 “Kama vyanzo hivi visingeingizwa basi kiwango hicho kisingefikiwa. TRA hawajapanua wigo wa ukusanyaji mapato. Chanzo pekee kilichoboreshwa ni kodi ya mafuta,” amesema Silinde ambaye ni naibu waziri kivuli wa fedha.