TRA yaagiza maduka yaliyofungwa Mtwara kufunguliwa

Muktasari:

Maduka hayo yalifungwa kutokana na sababu mbalimbali


Mtwara. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagiza maduka yote yaliyofungwa na mamlaka hizo kutokana na sababu mbalimbali kufunguliwa.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Machi 19, 2018 mkurugenzi wa elimu ya mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema tamko hilo limetolewa Jumamosi Machi 17, 2018.

Alipoulizwa sababu za maduka hayo kufungwa na TRA amesema: “Wewe unapaswa kutambua kuwa maduka hayo tumeyafungua yaendelee kufanya shughuli zake. Hayo ambao  yalifungiwa kwa sababu gani si sahihi sana kwa sasa. Kama kuna waliofunga wenyewe kwa sababu zao, hatuwezi kuwataka wafungue na kuendelea na shughuli zao.”

Meneja msaidizi wa ukaguzi TRA, Patrick Mateni aliieleza MCL Digital wiki moja iliyopita kuwa operesheni ya kufunga maduka ambayo hayatumii mashine za kielektroniki ni endelevu ikiwamo kuwafungia wote ambao hawajalipa kodi.

Alizitaja biashara zilizofungiwa kwa kutokutumia mashine za EFD kuwa ni maduka ya simu na kituo kimoja cha redio.

 “Hili zoezi ni endelevu si kwamba tunafunga tu bila sababu, kwanza tunafunga kutokana na mfanyabiashara kukiuka  taratibu za sheria ya kodi. Kila mmoja alikuwa na tatizo lake katika masuala ya kodi,” amesema.