Tuesday, February 13, 2018

VIDEO-TRA yakamata madumu 500 ya mafuta kwa kutolipa kodi

By Lilian Lucas, Mwananchi llucas@mwananchi.co.tz

Morogoro. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imekamata madumu 500 ya mafuta ya kula yakisafirishwa kwenda mikoa ya kanda ya nyanda za juu kusini yakitokea mkoani Tanga bila kuwa na risiti za mashine za kielektroniki (EFD).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 13, 2018, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Maternus Shirima amesema maofisa wa mamlaka hiyo wakiwa katika operesheni ya kawaida katika maeneo ya mbalimbali waligundua kuwepo kwa lori lenye mafuta ambayo yalikuwa hayajalipiwa kodi wala kutolewa risiti.

Amesema baada ya kukamatwa kwa lori hilo mamlaka hiyo imeanza kuchukua hatua kwa wauzaji na wanunuzi ili kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria huku wakitakiwa kulipa kodi.

Amebainisha kuwa kwa sasa kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya wanunuzi na wauzaji bidhaa kushirikiana kukwepa kulipa kodi kwa kuandikiana risiti kwa kiwango kidogo cha fedha.

Meneja huyo amesema kufanya hivyo ni sawa na kuiibia Serikali na kuikosesha mapato.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya ulipaji kodi na kudai risiti, inapotokea mtu anakiuka huwa tunachukua hatua dhidi yake kwa mujibu wa sheria yetu,” amesema.

Ofisa Kodi wa TRA, Peter Jacob amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanaponunua na kuuza bidhaa watoe risiti.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya adhabu ya TRA, mtu yeyote atakayekamatwa kwa kutolipa kodi ama kutoa risiti adhabu anakabiliwa na kifungo cha miaka mitatu au kulipa Sh4.5 milioni ama adhabu zote kwa pamoja.


-->