TRA yakusanya Sh11 trilioni kwa miezi tisa

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza na waadishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar ea Salaam. Kwa robo tatu za mwaka wa fedha wa 2017/2018, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh11.78 trilioni kati ya Sh17.1 trilioni zinazotarajiwa.

Kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.8 au theluthi mbili ya matarajio ikilinganishwa na asilimia 71.9 ya matarajio ya kipindi kama hicho mwaka jana.

Mwaka 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya Sh15.1 trilioni lakini kwa miezi tisa ya kwanza ilifanikiwa kupata Sh10.86 trilioni na miezi 12 ilipokamilika ilikusanya Sh14.4 trilioni hivyo kuwa na upungufu wa Sh700 bilioni.

Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema licha ya mwenendo huo, bado kuna matumaini ya kufikia malengo yaliyowekwa.

“Makusanyo yameongezeka kwa asilimia 8.46 ikilinganishwa na Sh10.86 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita wa fedha,” alisema Kayombo.

Taarifa ya TRA kwa umma inaeleza mwenendo wa makusanyo ulitofautiana kati ya mwezi mmoja na mwingine.

Katika miezi iliyokuwa na makusanyo makubwa, taarifa inaonyesha Desemba mwaka jana mapato yaliongezeka kwa asilimia 15.58 kutoka Sh1.41 trilioni hadi Sh1.63 trilioni mwaka huu, huku yale ya Machi yakipanda kwa asilimia 14.49 kutoka Sh1.34 trilioni kwa mwaka uliopita hadi Sh1.54.

Inaendelea kueleza kwamba Septemba ndio mwezi ambao haukufanya vizuri kuliko yote kwani makusanyo yalipungua kwa asilimia 2.37 kutoka Sh1.37 trilioni mwaka uliopita hadi Sh1.34 mwaka huu.

Kayombo alisema mafanikio ya makusanyo yaliyopatikana yamechangiwa na ushirikiano na utayari wa wafanyabiashara, watumishi wa TRA, hamasa iliyotolewa na viongozi wa Serikali pamoja na mchango wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi.