VIDEO: TRA yashindwa kufikia lengo ukusanyaji wa kodi mwaka 2017/18

Muktasari:

Imesema licha ya kutofikia lengo, imeongeza makusanyo kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa asilimia 7.5

Dar es Salaam. Licha ya kutofikia lengo la makusanyo ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza makusanyo yake katika mwaka huo kwa asilimia 7.5 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017.

Katika bajeti kuu ya Serikali mwaka 2017/18, chombo hicho kikuu cha ukusanyaji wa kodi kililenga kukusanya Sh17.1 trilioni, lakini mpaka mwaka unaisha fedha zilizokusanywa ni Sh15.5 trilioni, kukiwa na pungufu ya Sh1.6 trilioni.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 16, 2018, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema mafanikio hayo yametokana na kampeni ya uandikishaji walipakodi pamoja na elimu ya kodi kuendelea kueleweka kwa wananchi.

 

"Tumedhamiria kuongeza kasi ya usajili wa walipa kodi wapya ili kila mtu anayestahili kulipa kodi asajiliwe na kuchangia maendeleo ya Taifa. Tunawapongeza walipakodi wote kwani ndio wanaosaidia Serikali kutekeleza mipango yake ya kuimarisha uchumi na kutoa huduma kwa wananchi," amesema Kayombo.

 

Aidha,  katika taarifa ya makusanyo ya mwaka mzima iliyotolewa leo, Desemba 2017 ndiyo uliongoza kwa makusanyo ya Sh1.63 trilioni huku Aprili, 2018 zikikusanywa zaidi ya Sh1.07 trilioni.