TTB yaitia kitanzini TLTC kwa ukaidi

Muktasari:

Akitoa maazimio ya kikao cha bodi kilichoketi juzi, Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kampuni hiyo kutakiwa kufanya malipo hayo, lakini ilikaidi.

Tabora. Bodi ya Tumbaku nchini (TTB), imesitisha leseni zote za biashara za kampuni kubwa ya ununuzi wa tumbaku ya TLTC zilizotolewa na bodi hiyo, kutokana na kukaidi maagizo ya Serikali kulipa fedha za malipo ya pili wanazodaiwa na wakulima.

Akitoa maazimio ya kikao cha bodi kilichoketi juzi, Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kampuni hiyo kutakiwa kufanya malipo hayo, lakini ilikaidi.

“Hata Serikali iliitaka iwalipe wakulima, lakini hawakusikia na bado hawajajibu kitu hadi sasa,” alisema Kawawa.

Alisema kwamba, leseni za biashara za TLTC zitaendelea kusitishwa hadi itakapowalipa wakulima malipo yao ya pili ambayo hakuyataja kiasi chake.

Mbali ya hatua hiyo pia alisema bodi yake imeziagiza kampuni zingine za ununuzi wa tumbaku za Alliance One, JTI na PATL zilizoonyesha nia ya kuwalipa wakulima, kufanya hivyo ndani ya siku saba kuanzia juzi.