TWB yatoa siku saba wadaiwa sugu 7,000 kulipa madeni la sivyo..

Mwenyiki wa Bodi ya Benki ya Wanawake, Beng’i Issa

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Beng’i Issa alisema uamuzi huo ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la mikopo chechefu au isiyolipika.

 Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) imetangaza kuzipiga mnada mali za wadaiwa sugu 7,065 watakaoshindwa kulipa madeni yao ndani ya siku saba kuanzia leo.

Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Beng’i Issa alisema uamuzi huo ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la mikopo chechefu au isiyolipika.

“Mpaka sasa mikopo isiyolipika imefikia Sh7.9 bilioni hivyo kuongeza ugumu kidogo katika kuhakikisha tunapata mtaji wa kutosha,” alisema Issa.

Ndani ya muda walioutoa, alisema wateja wanaodaiwa wanapaswa kulipa madeni yao ambayo ni ya muda mrefu.

“Wengi wameshapitiliza siku 90 za kutorejesha madeni yao kinyume na utaratibu na makubaliano na benki,” alisema Issa.

Kwa watakaoshindwa kulipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa wa benki kuchukua hatua za kisheria kabla ya kunadisha dhamana zao, alisema wenye dhamira ya kulipa waende kwenye tawi lolote la benki hiyo wakiwa na mpango mahususi wa jinsi watakavyofanikisha malipo yao.

Januari 4, wakati Benki Kuu Tanzania (BoT) ikitangaza kufuta leseni za baadhi ya benki nchini, TWB ilipewa agizo la kuongeza mtaji ndani ya miezi sita ili kukidhi mahitaji ya ukwasi unaohitajika.

Kulingana na masharti ya taasisi za fedha na benki za biashara nchini, kila moja inatakiwa kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi mahitaji ya kila siku.

Wakati TWB ikipewa onyo hilo, Benki ya Covenant, Efatha, Benki ya Wananchi Njombe, Kagera Farmer’s Cooperative Bank na Benki ya Wananchi Meru zilifutiwa leseni.

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Japhet Justine alisema sheria inawaruhusu kuuza mali au dhamana za wateja walizoweka endapo watashindwa kurejesha mkopo kwa wakati waliokubaliana.

“Mbali na kupiga mnada mali zao, taarifa zao tutazipeleka Benki Kuu ya Tanzania wasiweze kupata mkopo katika benki nyingine yoyote nchini,” alisema Justine.

Alisema tangu kutolewa kwa taarifa ya awali kuwa benki ipo katika hali mbaya, wamekusanya zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa wadaiwa walionao, hatua ambayo alisema ni nzuri.

Kwa sasa, alisema wapo katika mazungumzo na wadau mbalimbali ili kupata mtaji waliowekewa na BoT na kwamba muelekeo unaonekana kuwa mzuri.

“Baada ya benki yetu kupewa maagizo ya kuongeza mtaji na Benki Kuu tunapokea wateja na wageni wengi wanaohitaji ufafanuzi kuhusu fedha zao lakini wote wanaelewa,” aliongeza.