Taarifa ya mbunge Siha kujiuzulu pasua kichwa

Muktasari:

  • Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro asema chama hakina taarifa.

Barua na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza mbunge wa Siha (Chadema) mkoani Kilimanjaro, Dk Godwin Mollel amejiuzulu ubunge imezua mjadala.

Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema akizungumza na MCL Digital leo Alhamisi Desemba 14,2017 amesema naye ameona video na barua kwenye mitandao ya kijamii lakini hawana uthibitisho wowote.

"Mheshimiwa Mollel hakuwahi kuonyesha dalili yoyote kuwa yuko kwenye hilo wimbi na mimi nimeona hiyo barua na video kwenye mitandao. Bado kwangu nachukulia kama uvumi mpaka tutakapothibitisha," amesema.

Lema amesema kwa utaratibu alipaswa kumuandikia barua Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe au viongozi wa Chadema.

Amesema akiwa katibu wa mkoa wa chama hicho hajapokea barua yoyote kutoka kwa Dk Mollel.

"Ukiangalia hata barua inayosambaa haijasainiwa na video inaonyesha ni mtu tu kajirekodi akarusha. Katika mazingira hayo hatuwezi kukurupuka kuzungumzia hilo jambo," amesema.

Taarifa inayosambaa kwenye mitandao ambayo haina saini inaonyesha kuandikwa na Dk Mollel akieleza ameamua kujivua uanachama wa Chadema kuanzia leo Alhamisi Desemba 14,2017.

Pia, ametangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge na kwamba huo ni uamuzi wake alioufanya akiwa na akili timamu na hajashinikizwa na mtu yeyote.