Taasisi yamsafisha Banda kashfa ya ufisadi

Muktasari:

Banda akiwa bado madarakani, aliamuru ufanyike uchunguzi huru kuhusu kufichuka kwa ufisadi huo na ulifanywa na Kampuni ya Uhasibu ya Uingereza RSM (zamani ikiitwa Baker Tilly). Matokeo ya uchunguzi huo yalitolewa mwaka 2014.

Blantyre, Malawi. Mkurugenzi wa Tasisi ya Kupambana na Rushwa (ACB) Reyneck Matemba amesema ofisi yake haina ushahidi unaomhusisha aliyekuwa Rais wa Malawi Joyce Banda katika kashfa ya ufisadi ya Cashgate kuhusu uporaji wa raslimali za taifa ambayo ilifichuliwa chini ya utawala wake mwaka 2013.

Banda akiwa bado madarakani, aliamuru ufanyike uchunguzi huru kuhusu kufichuka kwa ufisadi huo na ulifanywa na Kampuni ya Uhasibu ya Uingereza RSM (zamani ikiitwa Baker Tilly). Matokeo ya uchunguzi huo yalitolewa mwaka 2014.

Matemba aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa Alhamisi kwamba kampuni hiyo ya uhasibu kamwe haikumhusisha Banda katika ufisadi.

Alisema katika uchunguzi wao hawajapata ushahidi unaoshikika juu ya Banda, akisema walichonacho ni maelezo yaliyorekodiwa ya watuhumiwa wa kashfa hiyo: Oswald Lutepo, Leonard Kalonga na hayati Treaser Senzani.

Alipoulizwa kuhusu maelezo ya polisi kwamba wamepata kibali kutoka serikali kwa ajili ya kumkamata Banda, kiongozi huyo wa ACB alisema Polisi wa Idara ya Fedha wamekuwa wakifanya uchunguzi kuhusu uhalifu unaohusiana na fedha. "Wao wanafanya uchunguzi kivyao,” alisema.

Mwaka jana, ofisa mawasiliano wa jeshi la polisi James Kadadzera alisema wamepata idhini ya kumkamatwa Banda.

"Ushahidi uliokusanywa unatosha kutumika kutilia shaha kwamba rais wa zamani alitenda makossa yanayohusiana na matumizi mabaya ya ofisi na utakatishaji fedha,” ilisema taarifa ya Kadadzera.