Taasisi zakabidhiwa historia ya Tanganyika

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya Kavazi LA Mwalimu Nyerere Profesa Saida Yahya akipokea nyaraka zenye kumbukumbu ya Tanganyika kutoka kwa Urmila Jhaveri.

Muktasari:

  • Nyaraka hizo zimetakiwa kutumika kama kumbukumbu kwa Taifa

Dar es Salaam. Taasisi tatu leo zimekabidhiwa nyaraka zinazoelezea historia ya Tanganyika sasa Tanzania.

Nyaraka hizo zilizokabidhiwa zinaonyesha  kumbukumbu za matukio yaliyotokea zaidi ya miaka 50 iliyopita zikielezea mapambano ya uhuru yalivyokuwa.

Taasisi zilizopokea nyaraka hizo ni Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Kavazi la Mwalimu Nyerere na National Archives.

Nyaraka  hizo zilikabidhiwa na Urmila Jhaveri mke wa marehemu  Jhaveri  Laxmichand, kiongozi wa kisiasa wa muda mrefu aliyekuwa na jukumu kubwa katika mapambano ya uhuru wa nchi, akishirikiana na Hayati Mwalimu Nyerere.
"Nyaraka hizi na picha zinaendelea kwa undani maendeleo ya kisiasa yalivyokuwa wakati ule na jinsi mume wangu alivyokuwa anachangamana na jamii nyingine," alisema  Urmila.

Naye aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini India Gertrude Mongela wanakati anapokea nyaraka hizo kwa niaba ya mfuko wa Mwalimu Nyerere amesema  anaamini zitakifundisha kizazi kilichopo na kijacho harakati za ukombozi wa nchi hii zilikuwa.

"Ninakubali mchango mkubwa wa mume wake kwa kuzingatia na kuona umuhimu wa kutunza barua, picha na nyaraka mbalimbali zinazohusu Tanganyika-Tanzania," amesema.

“Zinaeleza kuhusu Tanganyika na baadaye Tanzania zina picha na zikiwa katika mfumo wa video, inaonyesha ni kwa jinsi gani familia ya Jhaveri imethamini jambo hili, ”amesema Mongela.

Kwa upande wake, Mboneko Munyanga, aliyezungumza kwa niaba ya  familia ya Mwalimu Nyerere amesema "Tunaamini nyaraka hizi sio tu mchango muhimu kwa taasisi hizi tatu, lakini pia ni muhimu kwa ya historia ya nchi yetu."

Ameongeza "kizazi cha sasa kinakosa kumbukumbu muhimu za nchi hii, kupitia nyaraka hizi kuna jambo jipya watajifunza, "

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa  Saida Yahya amesema licha ya kutunza nyaraka hizo pia wameonyesha uzalendo na umoja.

Alifafanua Tanzania ni nchi isiyokuwa na matabaka na umoja huo ndiyo umezaa matunda ya kupata nyaraka muhimu kama hizo.

Amesema ni vema kizazi cha sasa kikaiga mfano huo kwa kuandika matukio muhimu na kuyatunza kwa ajili ya kizazi kijacho.

Balozi wa Mashariki ya Kati na Kusini mwa Afrika, Matthew Beeki-Uwiafo alimsifia  Urmila kwa kusimamia hati za kihistoria ambazo zilionekana kuwa muhimu katika rekodi ya historia ya nchi, hata baada ya mumewe kufariki mwaka 2004.

Hayati Jhaveri Laxmichand alikuwa kiongozi wa kisiasa hapa nchini na alikuwa miongoni mwa wanaharakati waliokuwa bega kwa bega na wapigania uhuru.

Amefariki nchini India mwaka 2004 baada ya kuugua na kwenda kutafuta matibabu. Mkewe Urmila alilazimika kurudi nchini kwa ajili ya kukabidhi nyaraka mbalimbali