Taji la Miss Tanzania hili hapa

Muktasari:

Mkurugenzi wa kampuni ya Look inayoendesha mashindano hayo, Basila Mwanukuzi amelionyesha taji hilo leo Agosti 27, 2018 mbele ya waandishi wa habari na kusema lina thamani ya Sh6 milioni.

Dar es Salaam. Ikiwa zimesalia siku 10 kabla ya kufanyika kwa shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania, kamati inayoendesha shindano hilo imeweka wazi taji atakalovikwa mshindi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Look inayoendesha mashindano hayo, Basila Mwanukuzi amelionyesha taji hilo leo Agosti 27, 2018 mbele ya waandishi wa habari na kusema lina thamani ya Sh6 milioni.

Amesema sanjari na taji hilo, mrembo atakayeibuka kidedea kwenye shindano hilo litakalofanyika Septemba 8 katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam atapewa zawadi ya gari.

Mwanukuzi amesema kamati yake imeendelea kusimamia na kuhakikisha mrembo anapata zawadi bora na yenye viwango.

Amesema kulingana na maandalizi ya kamati hiyo, mshindi atapewa gari zuri ambalo hata hivyo hakuweka wazi aina ya gari.

Kando na hilo, amesema tiketi za mwaka huu zitauzwa kwa mfumo wa kielektroniki.

Meneja masoko wa kampuni ya Otapp inayohusika na uuzaji wa tiketi hizo, Joachim Ferdinand amesema tayari tiketi timeanza kuuzwa.