Takriban Sh32 trilioni zinahitajika kuufikia uchumi wa viwanda

Muktasari:

  • Baada ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuandaa jukwaa la kwanza la fikra lililofanyika Juni likijadili magonjwa yasiyoambukiza, MCL inakuletea jukwaa la pili la fikra litakalofanyika katika ukumbi wa Kisenga, Kijitonyama, Oktoba 4, kujadili fursa na changamoto kuelekea Tanzania ya viwanda.
  • Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala zinazobainisha fursa na changamoto zilizopo. Leo tunakuletea uwekezaji unaohitajika kufanyika kufanikisha ndoto hiyo.

Kuipata Tanzania yenye uchumi wa kati unaotegemea viwanda mwaka 2025, zaidi ya Dola 14.1 bilioni za Marekani (sawa na Sh31.8 trilioni) zinahitajika kuwekezwa kwenye miradi ya kimkakati.

Kiasi hicho kinadhihirishwa na ukokotozi uliofanywa na gazeti hili kutokana na taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Jarida la miradi la kituo hicho liitwalo: ‘2018 Project Briefs on Selected Investment Opportunities’ limeainisha miradi 30 ambayo kiasi hicho kikiwekezwa itarahisisha kufanikisha safari ya Tanzania kubadili uchumi wake.

Miradi hiyo inajumuisha sekta ya mafuta inayohitaji Dola 8.96 bilioni) sawa na Sh20.2 trilioni) na ya gesi inayotaka Dola 3.61 bilioni (Sh8.158 trilioni). Kwenye viwanda vya bidhaa, kinahitajika kiasi cha Dola 895.59 milioni (Sh2 trilioni) huku miundombinu ya kiuchumi ikihitaji Dola 637.35 milioni (Sh1.4 trilioni) na madini Dola 4.5 milioni (Sh10.17 bilioni).

Mradi unaohitaji fedha nyingi zaidi kwenye sekta ya gesi ni ule uliopo kitalu 4/1B unaotarajiwa kusambaza nishati hiyo nchini, ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kusafirisha ughaibuni unaohitaji Dola 7.3 bilioni.

Kwenye gesi ni uzalishaji wa umeme wa megawati 600 katika Ziwa Ngozi huko mkoani Mbeya kutakakowekezwa Dola 821 milioni. Mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili; ya kwanza ikizalisha megawati 200 na ya pili kiasi kinachobaki.

Wilayani Monduli, jarida hilo linasema kutakuwa na kiwanda cha magadi kitakachojengwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa ubia na sekta binafsi kwa gharama ya Dola 750 milioni.

Ujenzi wa bandari ya uvuvi itakayojengwa kwenye moja ya wilaya 16 za pwani kuanzia Tanga mpaka Mtwara na kugharimu Dola 600 milioni unaelezwa kuwa mradi ghali zaidi kwenye miundombinu inayohitaji kujengwa kutekeleza nia ya Serikali kwa wakati.

Mkoani Kagera, mradi wa machimbo ya bati uliopo Kyerwa unatarajia kusambaza bidhaa hiyo kwa wazalishaji wa ndani endapo Dola 4.5 milioni zitawekezwa.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Geoffrey Mwambe anasema hilo litawezekana endapo kutakuwa na ubia katika uwekezaji kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).

“Milango ipo wazi kwa wawekezaji. Ni kupitia viwanda pekee Tanzania inaweza kutimiza ndoto ya kukuza uchumi wake kwa kuanza kusafirisha bidhaa badala ya malighafi,” anasema Mwambe.

Uwekezaji huo, anasema utasaidia kukuza ajira mpya kwa mwaka, kupanua masoko ya bidhaa za kilimo na kukuza kipato cha wawekezaji, wananchi hata mapato ya Serikali.

Kutokana na sababu tofauti, Tanzania inaelezwa kuongoza kuvutia uwekezaji ikilinganishwa na majirani zake wa Afrika Mashariki (EAC). Ripoti ya uwekezaji kwa mwaka 2017 ya Benki ya Dunia inabainisha hilo.

Si hiyo pekee, utafiti wa Benki ya Rand Merchant Bank (RMB) ya Afrika Kusini ya mwaka 2016 uliiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 za Afrika zinazovutia zaidi kwa uwekezaji.

“Wawekezaji wanaovutiwa kuja Afrika Mashariki au Afrika kwa ujumla wanapaswa kuelewa mazingira na mvuto wa Tanzania. Ni nchi kubwa na yenye watu wengi zaidi kwa ukanda huu,” anasema Mwambe.

Tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amekuwa akisistiza ujenzi wa viwanda ili kuchochea uchumi wa Taifa.

Kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki, Rais anapambana na rushwa na ufisadi, urasimu na uzembe kazini hasa kwa watumishi wa umma. Kuongeza umakini zaidi, Serikali imezuia matumizi ya mitandao ya kijamii muda wa kazi.

Dk Magufuli ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na sekta binafsi ambayo ni mdau mkubwa wa kufanikisha ujenzi wa viwanda. Kuongeza uharakishaji wa mchakato huo, Rais anahimiza nidhani ya kazi kwa watumishi wote.

Kuunga mkono juhudi hizo, TIC imekuwa ikiratibu na kuendesha kampeni kadhaa za kuhamasisha uwekezaji na kukuza soko la bidhaa za nchini kwa kushawishi wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa zilizopo.

Ni juhudi ambazo hazijapoteza bure nguvu za wahusika kwani kampuni kadhaa za ndani na nje zimejitokeza. “Tukiwa wakala wa kwanza kuhamasisha uwekezaji, kituo kinaangalia namna ya kuwavutia wawekezaji wakubwa na kuwahakikishia usalama wa miradi yao,” anasema mkurugenzi huyo wa kituo cha uwekezaji.

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ipo tayari kushiriki kwenye utekelezaji wa sera hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Godfrey Simbeye anasema miradi mikubwa inahitaji fedha nyingi ambazo ni changamoto kwa wajasiriamali waliopo ambao wana mtaji mdogo huku benki za biashara zikiwa hazitoi mikopo mikubwa ya muda mrefu.

Kuzikabili changamoto hizo, anaiomba Serikali kuzishawishi taaisi za kimataifa kuwakopesha wajasiriamali wadogo kwa udhamini wake (Serikali) kwa riba ndogo ili kuongeza ushiriki wao.

Kutokana na utayari wa Serkali kuishirikisha sekta binafsi kwenye miradi ya kimkakati, Simbeye anasema kwamba anaamini hiki ni kipindi cha mpito kinachowapa wafanyabiashara nafasi ya kujipanga na kuzichangamkia fursa za uchumi zilizopo.