Takukuru yaendelea na uchunguzi dhidi ya wanachama wa CCM

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale 

Muktasari:

Takukuru imesema inaendelea kukusanya ushahidi ili kuwafikisha mahakamani au kuwaachia viongozi na makada wa CCM.

Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, imeendelea kuwang’ang’ania viongozi na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendeleza uchunguzi dhidi yao kuhusu tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi uliomalizika Desemba 3,2017.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale leo Alhamisi Desemba 7,2017 ameieleza MCL Digital kuwa taasisi hiyo inaendelea kukusanya ushahidi ili kuwafikisha mahakamani au kuwaachia viongozi na makada hao ambao hata hivyo hakuwa tayari kuwataja.

“Ninachoweza kukuthibitishia ni kwamba, tunaendelea na uchunguzi; ukikamilika tutawajulisha na hatua zingine za kisheria zitafuata,” amesema Makale.

Desemba 2,2017 maofisa wa Takukuru wilayani Ukerewe walilikamata na kulipekua gari la Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo alipokuwa katika kampeni za kutetea nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Desemba 3,2017 katika uwanja wa CCM Kirumba.

Akiwahutubia wana CCM baada ya kutangazwa mshindi kwa kura 555 dhidi ya kura 520 za mshindani wake wa karibu Saidi Mecky Sadiki, Diallo alielezea kitendo cha gari lake kupekuliwa hakikuwa cha kiungwana kwa sababu yeye ni muumini wa vita dhidi ya rushwa ambayo ni adui wa haki kupitia imani na ahadi yake ya mwana CCM.

Siku ya uchaguzi, maofisa wa Takukuru waliwakamata viongozi wanne wa CCM kutoka wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kukutwa wakigawana Sh400,000 zikiaminika kuwa za rushwa kutoka kwa mmoja wa wagombea.

Makale alisema waliokamatwa, kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea ni Gabriel Gregory, diwani wa kata ya Bukindo na mwenzake, Nicholaus Munyoro wa kata ya Murutunguru; Steven Mzige, Mwenyekiti wa CCM kata ya Muriti na Katibu wa Uenezi wilayani Ukerewe, Musa Manka.