Takukuru yaweka kiporo rushwa ya wana CCM

Muktasari:

Bosi Takukuru aahidi kuanika uchunguzi siku atakayopanga

Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mwanza imewaweka kiporo viongozi na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuahirisha kutoa taarifa ya uchunguzi dhidi yao iliyopangwa kutolewa Januari 15.

Wanaochunguzwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM ni pamoja na katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Nicholaus Munyoro; diwani wa Kata ya Murutunguru, Musa Manka; diwani wa Kata ya Bukindo, Gabriel Gregory na Steven Mazige ambaye ni mwenyekiti wa CCM Kata ya Ukerewe.

Makada hao walitiwa mbaroni na Takukuru Desemba 2, 2017 wakati wa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa CCM mkoani Mwanza uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa madai ya kukutwa wakigawana Sh400, 000 zilizosadikiwa kuwa rushwa iliyotolewa na mmoja wa wagombea.

Akizungumza kwa njia ya simu jana kuhusu suala hilo, mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale alisema taasisi hiyo itapanga siku nyingine ya kutoa taarifa ya uchunguzi dhidi ya viongozi hao baada ya kushindwa kufanya hivyo Jumatatu iliyopita.

Desemba Mosi, mwaka jana, Takukuru pia ilikamata na kulichunguza gari la mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Antony Diallo kwa kile mkuu wa taasisi hiyo mkoani hapa alichosema ni kuchunguza tuhuma za rushwa wakati kiongozi huyo alipokuwa wilayani Ukerewe kwenye harakati za kampeni za kuwania nafasi hiyo.

Alipozungumzia gari lake kupekuliwa wakati akiomba kura siku ya uchaguzi Desemba 2, Diallo alisema licha ya kumvunjia haiba mbele ya umma, kitendo hicho pia kilimuumiza kwa kuwa yeye ni muumini wa vita dhidi ya rushwa kupitia ahadi yake ya mwana CCM.

Baada ya kuchaguliwa na kutetea nafasi yake, Diallo alitumia hotuba yake ya kushukuru kwa kuchaguliwa kuwaonya viongozi na mamlaka za dola kuacha kutumia nafasi zao kuingilia michakato ya uchaguzi ndani ya chama hicho.