Takwimu za vifo vya mama na mtoto kupitiwa upya

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Otilia Gowelle

Muktasari:

Serikali imebaini kuwa takwimu za zilizopo sasa hivi hazipo sahihi na zinaleta mkanganyiko kwa watumishi wanaohusika na ukusanyaji taarifa

Mbeya. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Ofisi  Taifa la Takwimu (NBS),  imesema itaanza kupitia upya  takwimu za vifo vya mama na mtoto zinazotolewa hapa nchini.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Otilia Gowelle alibainisha hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara hiyo wakati akifungua mkutano mkuu wa  18  wa mwaka  wa taifa kwa Wauguzi wenye Huduma Binafsi (PRINMAT) uliofanyikia Mji mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya.

Dk. Otilia amesema Serikali ilibaini kwamba takwimu zilizopo sasa hivi hazipo sahihi na zinaleta mkanganyiko kwa watumishi wanaohusika na ukusanyaji taarifa za takwimu hizo.

Ametolea mfano, kwamba katika wilaya zinatolewa takwimu za wanawake wajawazito 556 kati ya vizazi hai 100.000 wamekufa, takwimu hizo zimekuwa zikikwamisha jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia wizara hiyo za kupunguza vifo vya mama mjamzito na mtoto.

Awali, Mwenyekiti wa PRINMAT taifa, Keziah Kapesa  amesema  tangu PRINMAT kuanzishwa miaka 18 iliyopita ina vituo 115 katika mikoa 23 na hadi sasa hakuna vifo vyovyote vilivyotokea kwenye vituo vyao na lengo lake kuu ni kuongeza na kufikisha huduma bora za kitaalamu  kwa wananchi walio mbali na hospitali.