VIDEO-Tambwe Hiza wa Chadema alivyokufa ghafla

Muktasari:

  • Mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1959 alifariki ghafla nyumbani kwake eneo la Mbagala Kizuiani jana wakati akijaribu kuwahi hospitali kwa tatizo la pumu.

 Chadema imepata pigo baada ya kifo cha kada wake maarufu aliyekuwa kwenye timu ya kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni, Richard Hiza Tambwe.

Mwanasiasa huyo aliyezaliwa mwaka 1959 alifariki ghafla nyumbani kwake eneo la Mbagala Kizuiani jana wakati akijaribu kuwahi hospitali kwa tatizo la pumu.

Hiza aliyewahi pia kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi, CUF na CCM, mara ya mwisho alionekana jukwaani juzi jioni katika eneo la Tandale kwa Tumbo akiwa miongoni mwa wana Chadema waliokuwa wakimnadi mgombea ubunge katika Jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu.

Ndugu na wanasiasa waliozungumza na Mwananchi nyumbani kwa marehemu, walisema hadi juzi alipokuwa jukwaani akimnadi Mwalimu hakuonekana kuwa na tatizo lolote.

Katika kampeni hizo, Tambwe alitoa kauli mbalimbali ambazo jana baada ya taarifa za kifo chake kusambaa, ziliibua mjadala katika mitandao ya kijamii, wengi wakisema ni kama alitabiri kifo chake.

Mauti yalivyomkuta

Tambwe alifariki dunia akiwa katika maeneo ya nyumbani kwake, Mtaa wa Mkochea, Mbagala Kizuiani wakati akijaribu kuwahi hospitali baada ya kushikwa na pumu.

Habari zilizopatikana nyumbani kwa marehemu, zilieleza kuwa baada ya kuzidiwa, Tambwe alichukua gari ili kuwahi katika hospitali lakini alizidiwa na kushindwa kuendelea na safari akiwa katikati ya barabara nje ya makazi yake.

Ilielezwa kwamba dereva mmoja wa basi la wanafunzi ambaye hakufahamika jina lake aliyekuwa nyuma yake, alilazimika kuacha gari lake na kuendesha gari la Tambwe baada ya kumkuta akiwa amepoteza fahamu.

Jirani wa familia ya Tambwe, Ashura Said alisema, “Karudi jana (juzi) kutoka kwenye mihangaiko yake huko kama kawaida akiwa hana shida yoyote lakini usiku alianza kusumbuliwa na pumu, asubuhi aliamua kutoka na gari akashindwa. Alianza kuhangaika hapo getini, ikabidi tuombe msaada wa dereva kwa school bus aliyekuwa anapita, akajaribu kumuwahisha hospitali lakini kumbe alikuwa ameshafariki dunia, inasikitisha na inaumiza sana.”

Mtoto wake wa kiume, Tulo Tambwe alisema baba yake alifariki dunia dakika chache kabla ya kufikishwa katika Hospitali ya Kizuiani, iliyopo mita chache kutoka nyumbani kwake.

“Leo alfajiri saa 11:00 alipojisikia kubanwa na pumu, aliamka na kuchukua gari ili aende hospitali, alipoanza kutoka getini hapa nyumbani ili kuingia barabara ndogo, akashindwa kutoka, akaziba njia,” alisema. Tulo ambaye hakuwapo nyumbani wakati wa tukio hilo, alisema taarifa alizozipata asubuhi kutoka kwa mashuhuda zinaeleza jinsi dereva wa gari la kubeba wanafunzi alivyomsaidia baba yake hadi hospitalini.

“Dereva wa gari hilo hadi aliamua kuendesha gari lake (Tambwe) ili kumuwahisha hospitali ya jirani hapa Kizuiani, lakini kabla ya kufikika inasemekana alikuwa tayari ameshafariki,” alisema.

Tulo alisema ingawa Tambwe alikuwa akiishi na mkewe pamoja na mtoto nyumbani hapo, juzi usiku wakati akikutana na hali hiyo alikuwa peke yake.

Charles Tambwe ambaye ni mdogo wa marehemu alisema, kaka yao alikuwa akisumbiliwa na ugonjwa huo kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita na alikuwa anatumia dawa wakati wote.

Mwili wa mwanasiasa huyo uliohifadhiwa katika Hospitali ya Temeke utazikwa jijini Dar es Salaam siku itakayotangazwa hapo baadaye.

Baada ya kusambaa kwa taarifa za msiba huo, waombolezaji walianza kufika nyumbani kwa marehemu kufanya eneo hilo kutawaliwa na vilio hasa kutoka kwa majirani, ndugu, jamaa na viongozi wa kisiasa.

Wanasiasa wamzungumzia

Baadhi ya wanasiasa wa vyama mbalimbali walimzungumzia mwanasiasa huyo aliyekuwa machachari huku naibu katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa akisema alimfahamu kwa sifa kuu mbili; ujasiri wa kuzungumza alichokiamini na kupenda uhuru.

“Lakini pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi watu majukwaani kumsikiliza, alitumia lugha nyepesi zaidi ili kufikisha ujumbe na alikubalika sana, tumempoteza mwanasiasa makini na mjenzi wa demokrasia,” alisema Mtemelwa.

Mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano kwa umma, wa CUF, Abdul Kambaya alisema chama chake kitamuenzi Tambwe kwa mchango wake katika kukuza uhai wa chama hicho na demokrasia nchini.

Alisema Tambwe alikuwa mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama hicho tangu mwaka 1998 hadi 2005 alipojiunga na CCM.

“Unapozungumzia ukuaji wa chama, lazima utalitaja jina la Tambwe Hiza, tutamuenzi kwa mchango wake ndani ya chama, lakini hata katika ukuaji wa demokrasia nchini.

“Amefariki akiwa ni mwanasiasa anayeamini sana fikra zake zaidi kuliko vyama alivyokuwa akijiunga navyo, ndiyo sababu amehama vyama vinne vikubwa ndani ya miaka karibu 18,” alisema.

Katibu wa uenezi na itikadi wa CCM, Humphrey Polepole alisema marehemu Tambwe amemaliza mbio zake katika maisha ya siasa hapa nchini. Alisema CCM imepokea kwa masikitiko na inatoa pole kwa wanandugu na wapenda demokrasia wote nchini.

“Ninachoweza kusema ni kwamba Tambwe tambo amepiga, mwendo ameumaliza katika siasa za hapa nchini, CCM inatoa pole kwa ndugu, wanafamilia na wapenda demokrasia wote nchini, bwana ametoa na bwana ametwaa,” alisema.

Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema Taifa limepoteza nguvu kazi katika ujenzi wa demokrasia, ambayo bado ilikuwa inahitajika. Alisema katika maisha yake ya siasa, Tambwe alikuwa muwazi, alijua siasa za majukwaani na hata ushawishi wa kusikilizwa na watu.

“Ndani ya NCCR alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa chama, alipoondoka aliendelea kufanya siasa zisizokuwa na uadui, hii inatufundisha katika maisha ya siasa, hakuna anayeijua kesho. Sisi NCCR tunamuenzi kwa ustawi wa siasa zake, aliijua siasa ya Tanzania, alikuwa kiongozi na mwanasiasa aliyekomaa kwa kupita vyama vikubwa,” alisema Juju.