Tamwa yashangazwa na matukio ya ubakaji, ndoa za utotoni

Muktasari:

Imesema juhudi za makusudi baina ya wadau mbalimbali zinahitajika ili kutokomeza matukio hayo

Kisarawe. Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Eda Sanga amesema anashangazwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa wanawake na ubakaji nchini akisema Tanzania ya sasa imebadilika.

"Hii siyo Tanzania ninayoijua. Yalitokea huko nyuma lakini hii hali ya sasa unaona kabisa ile dhamira ya kibinadamu inakuwa haipo," amesema Eda

Amesema hayo leo Septemba 18,2018 wakati akifunga mkutano wa wadau kupinga ukatili wa kijinsia uliotoa maazimio ya namna ya kupambana na ukatili huo uliofanyika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Amesema Tanzania bila unyanyasaji na ukatili inawezekana na kuwataka wadau hao kuwa mabalozi wa kupinga ukatili ikiwamo ubakaji, ndoa za utotoni na ulawiti.

Awali, Mkuu wa  Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema wilaya hiyo ina idadi kubwa ya matukio ya ubakaji. Amesema kesi za ubakaji hasa kwa watoto ni nyingi  wilayani humo.

Ameitaka Tamwa kutoa elimu ili kumaliza matukio ya ubakaji na ndoa za utotoni.