Tamwa yazindua mradi wa usalama barabarani

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga

Muktasari:

Mradi huo ulizinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga.

Dar es Salaam. Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimezindua mradi unaolenga kuwaepusha wanawake na watoto kuepukana na ajali za barabarani.

Mradi huo ulizinduliwa jana jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga alisema wameanzisha mradi huo ambao utawashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari katika kuufanikisha.

Sanga alisema baada ya kubaini wanawake wengi na watoto wanaendelea kuangamia kwa ajali za barabarani zinazotokea kila siku nchini hawakutaka kukaa kimya.

“Na Lengo mradi wetu ni kutoa elimu ya usalama barabarani kwa njia mbalimbali na tutajikita katika kutoa elimu ya makatazo kwenye vipengele vitano,” alisema Sanga.

Alivitaja kuwa ni pamoja na  athari ya ulevi kwa dereva anapokuwa anaendesha gari, umuhimu wa kuvaa kofia ngumu kwa madereva wa bodaboda na abiria na kufunga mikanda katika mabasi na magari madogo.