Tanesco K’njaro yatoa tahadhari kuhusu nyaya

Muktasari:

  • Tanesco pia imewatahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya mafundi bandia (vishoka) wanaowaunganishia umeme bila kuwa na utaalamu.

Moshi. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limewataka wananchi kuchukua tahadhari za kiusalama kwa kufanya ukaguzi wa mifumo ya nyaya iliyomo katika majengo yao kila baada ya miaka mitano.

Tanesco pia imewatahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya mafundi bandia (vishoka) wanaowaunganishia umeme bila kuwa na utaalamu.

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa Kilimanjaro, Samwel Mandari alitoa tahadhari hiyo mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea athari za kutokagua mifumo ya nyaya za umeme.

Mandari alisema mwaka huu zimetokea ajali kubwa nne za moto zilizosababisha vifo vya watu wanne na ajali ndogo 20 za nyumba kuungua zilizotokana na kuchakaa kwa miundombinu hiyo.

Alisema zipo shughuli za binadamu zinazoathiri miundombinu akiwataka wananchi kuepuka kupanda miti karibu na miundombinu ya umeme.

Mhandisi wa matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya umeme mkoani Kilimanjaro, Renatus Mwanga aliwataka wananchi kuwa makini wakati wa ujenzi wa majengo yao.