Tanesco Mwanza kukomalia deni la Sh4.5 bilioni

Muktasari:

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Mwanza, Flaviana Moshi amesema katika kundi hilo kuna taasisi za umma na watu binafsi.

Wakati notisi ya siku 14 iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhusiana na wadaiwa sugu kuwa wamelipa inamalizika leo, mkoani Mwanza wadaiwa wana Sh4.5 bilioni za shirika hilo.

Ofisa Uhusiano wa Tanesco Mkoa wa Mwanza, Flaviana Moshi amesema katika kundi hilo kuna taasisi za umma na watu binafsi.

Amesema tabia ya wateja kushindwa kulipa madeni yao kwa wakati wanalifanya shirika hilo lishindwe kukamilisha kazi zake au kukwama kabisa.

Hata hivyo, wakati Tanesco inakusudia kuanza leo kuchukua hatua dhidi ya wateja wake wasiolipa madeni, Meneja Mkuu wa Pepsi (SBC) nchini, Nico Coetzer ameitaka kujiridhisha kabla ya kutekeleza uamuzi huo ili usilete athari hasa katika maeneo yanayotoa huduma za afya, maji na viwanda.

Pia, ameshauri kutolewa kwa muda zaidi kwa wadaiwa hao badala ya kuwakatia umeme ambao ungeweza kuwasaidia kuendelea na uzalishaji utakaowasaidia kulipa madeni yao.