Tanesco yaidai JWTZ Sh3bilioni

Mkuu wa Majeshi nchini, Evance Mabeyo wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu  deni wanalodaiwa na Tanesco.Picha na Muyonga Jumanne

Muktasari:

  • Mabeyo ameyasema hayo leo wakati anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi (Ngome) na kueleza deni hilo limetokana na shughuli za jeshi hilo kwenye ulinzi wa Taifa pamoja na ufinyu wa bajeti.

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi nchini, Evance Mabeyo amesema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linadaiwa Sh3 bilioni na Shirika la Umeme nchini na kesho (Jumatatu)  watapunguza deni hilo ili wasikatiwe umeme.

Mabeyo ameyasema hayo leo wakati anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi (Ngome) na kueleza deni hilo limetokana na shughuli za jeshi hilo kwenye ulinzi wa Taifa pamoja na ufinyu wa bajeti.

"Baada ya kupokea maelezo ya Tanesco na kufuatia tamko la Rais, Jeshi la Wananchi limetafakari na limefanya jitihada kupata fedha za  kupunguza deni hili, tunadaiwa fedha kiasi kinachozi kidogo Sh3 bilioni, nimeagiza watendaji wetu watafute Sh1 bilioni," amesema Mabeyo.

Mabeyo amesema juhudi zinazofanywa na Jeshi hilo zinatakiwa kuonyeshwa na Taasisi nyingine ili kuweza kuiongezea Tanesco uwezo wa kutoa huduma.