Tanzania, Korea Kusini wasaini makubaliano

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini watakutana kesho Julai 23, 2018 

 

Dar es Salaam. Tanzania na Korea Kusini zimetia saini mkataba wa makubaliano ya kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili kwa kuondoa zuio la viza kwa watu wanaosafiri kidiplomasia na kiutumishi.

Mkataba huo umesainiwa leo Julai 22, 2018 wakati Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee Nak-yeon akiendelea na ziara nchini.

Lee amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akizungumza baada ya utiaji saini Ikulu jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema mkataba huo umelenga kuimarisha uhusiano, maendeleo ya kiuchumi, kiutamaduni na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

“Tumekaribisha kampuni nyingi kuja Tanzania kwa ajili ya uwekezaji na Watanzania mnajua tuna mradi mkubwa wa reli, tuna ujenzi wa daraja la Selander lakini pia tuna hospitali ya Mloganzila,” amesema.

Majaliwa amesema Serikali inatarajia kutekeleza miradi mingine mitatu mikubwa ukiwamo ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi mkoani Mwanza.

Amesema wafanyabiashara wa Tanzania na Korea Kusini watakutana kesho Julai 23, 2018 ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.

Majaliwa amesema Serikali ya Korea imekubali kutangaza vivutio vinavyopatikana nchini ili kuendelea sekta ya utalii.

“Waziri Mkuu, Lee ataendelea na ziara leo siku nzima. Atatembelea eneo la Nida kule Kibaha, atatembelea Makumbusho, anafurahia sana michoro ya tingatinga, anasema ni maarufu kule kwao lakini inapatikana Tanzania,” amesema Majaliwa.

Mwisho.