Tanzania, Mlima Kilimanjaro kuwania tuzo za vivutio vya utalii

Muktasari:

  • Tuzo zitatolewa Desemba 10 nchini Vietnam.

Dar es Salaam. Tanzania na Mlima Kilimanjaro imeorodheshwa kwenye tuzo za vivutio bora vya utalii zinazotarajiwa kutolewa Desemba.

Tuzo hizo zinazoandaliwa na Shirika la World Travel (WTO) ambazo zinatolewa kwa mara ya 24 mwaka huu, zimeiweka Tanzania kwenye kipengele cha nchi bora kuzitembelea kutokana na vivutio ilivyonavyo, wakati Mlima Kilimanjaro ukishindania kivutio bora cha utalii duniani.

Tuzo hizo zitakazotolewa kutokana na wingi wa kura ambazo kila kivutio kitapata kutoka kwa watalii, wataalamu wa sekta hiyo na watoa huduma, zitahitimishwa Desemba 10 nchini Vietnam.

Kwenye kipengele cha nchi yenye vivutio vingi, Tanzania inachuana na Botswana, Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Mlima Kilimanjaro unachuana na vivutio vingine vya jengo refu la Burj Khalifa (Dubai), Ferrari World (Abu Dhabi), The Great Wall (China) na Intramuros (Ufilipino).

Vivutio vingine vilivyo pamoja na mlima huo mrefu zaidi Afrika ni Las Vegas Strip (Nevada, Marekani), Machu Picchu (Peru), Spike Island (Ireland) na Mlima Sugarloaf.

Kupata ushindi, wadau wanatakiwa kujiandikisha na kupiga kura za kutosha kupitia tovuti ya waandaaji ambayo ni www.worldtravelawards.com/register.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Utalii nchini (TTB) imewaomba Watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kupiga kura kwa wingi ili vivutio hivyo vishinde na kubeba tuzo zilizoanzishwa mwaka 1983.

Sekta ya utalii nchini ilikua kwa asilimia 12.6 kati ya mwaka 2015 na 2016, hivyo kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa (GDP) licha ya ajira zaidi ya 500,000 inazotoa.

Huenda hali ikawa hivyo mwaka huu baada ya watu kadhaa maarufu duniani kutembelea vivutio vilivyopo nchini. Kwenye orodha hiyo wamo wanasoka, wanamuziki, waandishi wa habari na wanasiasa wa kimataifa.