Tanzania kuwa kinara uzalishaji wa maharage

Shamba la maharage

Arusha. Uzalishaji wa maharage bora unatarajiwa kuongezeka nchini na ifikapo mwaka 2020 ambao utaifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa makubwa barani Afrika yatakayoongoza kwa kuzalisha na kuuza nje kwa wingi.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Mazao ya Kilimo katika nchi za tropiki (CIAT), Jean Claude alitoa taarifa hiyo katika kikao cha wadau wa mbegu, kupitia mradi wa kusambaza mbegu bora za maharage nchini.

Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la kimataifa la Maendeleo la Marekani (Usaid) kupitia Shirika la mapinduzi ya kijani barani Afrika(AGRA).

Mahitaji ya mbegu bora za maharage nchini ni tani 125,000 kwa mwaka na wastani wa mbegu zilizozalishwa ni tani 51,812. Kuna upungufu wa tani 73,188 unaotarajiwa kuondolewa.

Claude alisema kuongezeka kwa uzalishaji wa maharage, kunatokana na kufanikiwa kwa mradi ulioanza mwaka 2015 wa kuzalisha mbegu bora, ambao ulianza kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kupitia Wakala wa Mbegu wa Serikali (ASA) na kampuni binafsi ya uzalishaji mbegu ya Meru Agro na Breeder Seeds. Alisema Wakala wa Serikali na kampuni hizo, ndani ya miaka miwili wameongeza uzalishaji wa mbegu za maharage kutoka wastani wa tani 10 kwa mwaka hadi kufikia tani 120 na tayari hekta 700 za mbegu za maharage zimeandaliwa.

Claude alisema kutokana na mradi huo, mavuno ya maharage kwa heka yameanza kuongezeka kutoka tani 1.5 hadi kufikia tani 1.8 na kwa kuwa Tanzania ina eneo la zaidi ya hekta 1.3 zinazofaa kulimwa Maharage, unatarajiwa kuongezeka zaidi.

Mtafiti kiongozi wa maharage nchini, Papias Binagwa alisema kwa sasa, katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kulima maharage kwa wingi.