Tanzania na Morocco kushirikiana kibiashara

Rais John Magufuli akiwa na Mfalme wa Morocco Mohammed VI

Muktasari:

Utiaji saini huo ulitokana na ujio wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, aliyeanza ziara ya kiserikali ya siku tatu juzi akiwa ameambatana na ujumbe wa zaidi ya watu 150 huku akiwa na msafara wa ndege tano.

Dar es Salaam.Tanzania na Morocco zimetiliana saini mikataba 21 ya kibiashara, ikiwamo ujenzi wa uwanja wa mpira  utakaogharimu dola za Marekani milioni 100.

Utiaji saini huo ulitokana na ujio wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, aliyeanza ziara ya kiserikali ya siku tatu juzi akiwa ameambatana na ujumbe wa zaidi ya watu 150 huku akiwa na msafara wa ndege tano.

Mikataba hiyo ilisainiwa jana Ikulu ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya mfalme huyo. Mbali na mikataba hiyo, wafanyabishara wa Morocco walifanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Tanzania kwa siku tatu mfululizo na kuhitimishwa jana.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema wamekubaliana kushirikiana katika sekta za biashara, kilimo, madini, uwekezaji na usafirishaji.

Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Morocco, Miriem Bensalah Chaqroun amesema Morocco ina teknolojia kubwa ya umeme wa nguvu za jua, hivyo ni fursa pia kwa Tanzania kugeukia mfumo huo wa nishati ili kuwa chanzo mbadala cha umeme.