Tanzania yachanua utawala bora ripoti ya Mo Ibrahim

Muktasari:

Viwango hivyo vilivyotolewa jana na ambavyo vimepima utendaji wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2012- 2016) vinaonyesha Tanzania imefanya vizuri. Maeneo yaliyotajwa kufanya vizuri na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya 17 miongoni mwa nchi 54 za Afrika ni yanayohusu amani, utawala wa sheria pamoja na utawala bora.

       Dar es Salaam. Tanzania imechanua na kufanya vizuri katika viwango vilivyotolewa na mfuko wa Mo Ibrahim uliopima hali ya utawala bora na maendeleo na kuziacha kwa mbali baadhi ya nchi za Afrika ikiwamo zile zilipo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC).

Viwango hivyo vilivyotolewa jana na ambavyo vimepima utendaji wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2012- 2016) vinaonyesha Tanzania imefanya vizuri. Maeneo yaliyotajwa kufanya vizuri na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya 17 miongoni mwa nchi 54 za Afrika ni yanayohusu amani, utawala wa sheria pamoja na utawala bora.

Ingawa ripoti hiyo ambayo ni ya 11 tangu mfuko huo uanze kutoa takwimu zake haikuonyesha Tanzania ilishika nafasi ya ngapi miaka ya nyuma lakini imeitaja kama nchi iliyofanikiwa kuvuka kiwango cha wastani kilichowekwa.

Ripoti inaonyesha kuwa Tanzania imepata alama 57.5 kati ya alama 100, ikiwa imepanda juu kiasi kutoka kiwango cha wastani ambacho ni alama 50. Eneo la utawala wa sheria, usalama wa taifa ndilo lilioipaisha zaidi Tanzania wakati ikifanya vibaya katika eneo linalohusu fursa za maendeleo endelevu na miundombinu.

Hata hivyo, ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Dakar, Senegal na kisha nakala yake kusambazwa kote Afrika imeonya juu ya mwendo wa kusuasua unaanza kujitokeza kwa baadhi ya nchi za Afrika.

“Kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyoanza kujitokeza katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, lakini kuna mwelekeo mpya usioridhisha unaoanza kuonekana na muhimu sasa kuchukuliwe tahadhari kuhusu hali ya baadaye ya bara hili,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Mfuko huo umezitambua nchi kama Ivory Coast, Morocco, Namibia, Nigeria na Senegal kuwa nchi ambazo siyo tu zimeendelea kutoa matumaini kwa wananchi wake, lakini ni mataifa machache barani Afrika ambayo yanapiga hatua yakisonga mbele.

Nchi kama Burundi, Cameroon, Libya na Msumbiji zimeorodheshwa katika ripoti hiyo kama mataifa ambayo yanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa amani.

Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo pia inazihimiza nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika miundombinu ya nishati ya umeme ikitiliwa wasiwasi hasa maeneo ya vijijini ambayo yapo katika hali ngumu.

Mfuko huo ambao ilianzishwa 2006 na bilionea mwenye asili ya Sudan mwenye uraia wa Uingereza, Mo Ibrahim umetaja maeneo kama ushiriki wa raia na haki za binadamu ni eneo ambalo limeimarika baada ya kushuhudiwa chaguzi nyingi zikifanyika katika mazingira ya uhuru wa uwazi. Hata hivyo, imeonyesha kuhusu mwenendo unaoanza kujitokeza kama vile vitendo vya kubinya uhuru wa kisiasa.