Tanzania yakanusha madai ya Kenya uchaguzi wa mwenyekiti AU

Mgombea huyo, Amina Mohammed ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alishindwa kwa tofauti ya kura tatu na mgombea kutoka Chad, Moussa Faki Mahamat katika uchaguzi huo uliofanyika mapema wiki hii jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Muktasari:

Dar es Salaam. Serikali imesema madai kuwa baadhi ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hayakumpigia kura mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kutoka Kenya, hayana ukweli.

Mgombea huyo, Amina Mohammed ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alishindwa kwa tofauti ya kura tatu na mgombea kutoka Chad, Moussa Faki Mahamat katika uchaguzi huo uliofanyika mapema wiki hii jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Uchaguzi huo ulihitimisha kampeni kali za viongozi wa mataifa hayo mawili. Wakati Rais Uhuru Kenyatta alituma ujumbe uliotembelea nchi zote wanachama wa AU, ziara za Rais wa Chad, Idris Deby ambaye alikuwa mwenyekiti wa AU katika baadhi ya nchi ilichukuliwa kuwa ni kampeni kwa mgombea wake.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Waziri Mohamed aliyepata kura 25 dhidi ya 28 za mpinzani wake, alizilaumu baadhi ya nchi jirani kwa kutompigia kura.

Awali, kulikuwa na ripoti zilizodai kuwa Burundi, Uganda na Djibout zilimpa kura zao Mahamat wakati Tanzania haikupiga kura yoyote.

Hata hivyo, akizungumza na BBC jijini Addis Ababa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Augustine Mahiga alisema madai yanayoendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya kuhusu uchaguzi huo hayana ukweli. “Kama (mgombea wa Chad) alipata kura nyingi katika awamu ya kwanza, basi hakuna wasiwasi wale kutoka katika ukanda wake walimpigia kwenye hatua iliyofuata,” alisema Mahiga.