Tanzania yalamba dume Uturuki

Rais John Magufuli na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan wakiwa wamenyanyua mikono juu ikiwa ni ishara ya furaha baada ya kusaini mikataba tisa ya ushirikiano katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbali na kusaini mikataba hiyo, wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki jana walikuwa na mazungumzo ya kujadili fursa zinazotokana na mikataba hiyo iliyosainiwa mbele ya Rais John Magufuli na mgeni wake, Rais Recep Tayyip Erdogan.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kunufaika katika Nyanja za utalii, elimu, viwanda, diplomasia, usafirishaji, utangazaji na afya baada ya kusaini mikataba tisa ya ushirikiano na Uturuki katika hafla iliyofanyika Ikulu jana.

Mbali na kusaini mikataba hiyo, wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki jana walikuwa na mazungumzo ya kujadili fursa zinazotokana na mikataba hiyo iliyosainiwa mbele ya Rais John Magufuli na mgeni wake, Rais Recep Tayyip Erdogan.

Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo kumuomba mgeni wake amsaidie ili benki ya Exim ya Uturuki iikopeshe Tanzania kwa ajili ya kugharamia kilomita 400 katika ujenzi wa reli ya kisasa.

Mgeni huyo pia alikuwa na ombi lake kwa Rais Magufuli, akitaka Tanzania isaidie katika kukabiliana na kikundi cha Fethullah Terror Organisation (Feto), ambacho alikielezea kuwa ni hatari kwa nchi zote na kukituhumu kuhusika katika jaribio lililoshindikana la kuipindua serikali yake.