VIDEO: Tanzania yatajwa kundi la pili hatarini kupata Ebola

Muktasari:

Ugonjwa wa Ebola uliwahi kulipuka mwaka 1976 Congo na kusababisha vifo vya watu 280 kati ya wagonjwa 316 waliobainika.


Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaja Tanzania kuwa katika kundi la pili la nchi zilizo katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Tathmini ya vihatarishi hivyo imeelezwa kuchangiwa na mwingiliano uliopo kibiashara, kijamii na kiuchumi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Brazzaville), ambayo ipo katika kundi la kwanza.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo Mei 25, Mwakilishi wa WHO nchini Uganda, Dk Miriam Nanyunja amesema shirika hilo limeziweka nchi katika makundi matatu kwa kuzingatia nchi ya Congo iliyoathirika na mwingiliano na nchi zinazoizunguka.

Amesema kumekuwa na mwingiliano wa usafirishaji, watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kukua kwa huduma za kiafya baina ya nchi moja na nyingine.

Amezitaja nchi zilizo katika kundi la pili kuwa ni Tanzania, Angola, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Zambia.

“Nchi iliyo katika kundi la tatu ni Uganda, ambayo yenyewe ipo kwenye hatari lakini kwa kuwa wao walishawahi kuwa na wagonjwa wa Ebola hapo nyuma angalau wana uwezo wa kukabiliana ikilinganishwa na nchi nyingine,” amesema.